Mkapa, Malecela waonyesha hisia zao kwa Mengi

Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela akisalimiana na
Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku (kushoto) walipokutana nyumbani kwa marehemu Reginald Mengi, Kinondoni jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni mke wa Malecela, Anne Kilango. Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Malecela aliyasema hayo jana alipofika nyumbani kwa Mengi, Kinondoni, Dar es Salaam ili kutoa rambirambi zake.

Kifo cha mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi kilichotokea juzi, Dubai katika Falme za Kiarabu (UAE), kimeendelea kuibua hisia za viongozi waliowahi kuwa karibu na mfanyabishara huyo enzi za uhai wake.

Tayari Rais John Magufuli na mtangulizi wake Jakaya Kikwete wamekwishaelezea namna walivyoguswa na msiba huo.

Viongozi hao walituma salamu zao za rambirambi juzi kupitia akaunti zao za Twitter.

Jana, Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa alituma salamu zake akisema Mengi alikuwa miongoni mwa Watanzania wachache waliokuwa wazalendo ambao Taifa halitawasahau.

“Nimemfahamu Mengi miaka mingi iliyopita na kwangu ananirudisha katika historia kama mzalendo aliyesimamia nafasi yake kwa jamii,” alisema Mkapa kupitia ujumbe wake wa rambirambi ambao Mwananchi lilipata nakala.

Alimtaja Mengi kuwa ni kati ya wazalendo wachache walioanzisha viwanda, aliyejitolea kwa ajili ya maisha ya wengine na kupambana kuondokana na umaskini ambaye Taifa litaendelea kujivunia.

“Wakati wa urais wangu, Dk Mengi kupitia shughuli mbalimbali alinifanya niwe Rais mzuri. Alikuwa mkweli katika maoni yake hata kama yalikuwa tofauti na misimamo yangu na hilo lilinifanya kufaidika na busara zake,” alisema Rais huyo mstaafu.

Alisema utumishi wa Mengi katika sekta binafsi umeendelea kuilea hadi leo na anatambulika kama mtu aliyemshawishi kila anayetamani kuona nchi ikiendelea.

Alisema namna pekee ya kumuenzi ni kufuata njia na mifano aliyoionyesha, kwamba kupambana na umaskini siyo jukumu la Serikali peke yake bali ni la kila mtu.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela alisema Mengi atabaki kwenye mioyo ya watu kutokana na mema aliyoyafanya.

Malecela aliyasema hayo jana alipofika nyumbani kwa Mengi, Kinondoni, Dar es Salaam ili kutoa rambirambi zake.

Alisema mtu anapotenda mema baada ya kufa hubaki kwenye mioyo ya watu, hivyo Mengi kutokana na mema aliyoyatenda ataendelea kukumbukwa.

Malecela alisema Mengi amefanya mambo mengi akigusa kila eneo la watu na kada zao, suala ambalo lilimfanya awe kimbilio la wengi.