Mkapa alivyomzungumzia Mengi

Muktasari:

  • Rais mstaafu wa awamu ya tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa ametoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha mfanyabiashara maarufu, Reginald Mengi aliyefariki usiku wa kuamkia jana Alhamisi akiwa Dubai.

Dar es Salaam. Rais mstaafu wa awamu ya tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa ametuma salamu zake za rambirambi kufuatia kifo cha mfanyabiashara maarufu, Regnald Mengi kilichotokea usiku wa kuamkia jana Dudai,  Umoja wa Falme za Kiarabu.

Katika salamu zale alizotuma kwenye vyombo vya habari leo Ijumaa Mei 3, Mkapa amemtaja Mengi kama miongoni mwa Watanzania wachache waliokuwa wazalendo ambao nchi haitawasahau.

“Nimemfahamu Mengi miaka mingi iliyopita na kwangu ananirudisha katika historia kama mzalendo aliyesimamia nafasi yake kwa jamii kwa ujumla,” amesema Mkapa katika salamu hizo.

Amemtaja pia Mengi kuwa kati ya wazalendo wachache walioanzisha viwanda, mtu aliyejitolea kwa ajili ya maisha ya wengine na aliyepambana kuondokana na umasikini.

“Wakati wa urais wangu, Dk Mengi kupitia shughuli mbalimbali alinifanya niwe Rais mzuri. Alikuwa mkweli katika maoni yake hata kama yalikuwa tofauti na misimamo yangu na hilo lilinifanya kufaidika na busara zake,” amesema.

Amesema utumishi wa marehemu Mengi anatambulika kama mtu aliyeshawishi kila mtu anayetamani kuona nchi ikiendelea.

Mkapa amesema njia pekee ya kumwenzi Mengi ni kufuata njia zake na mifano aliyoionyesha kwamba kupambana na umasikini siyo jukumu la Serikali pake yake bali ni kwa kila mtu.

“Tutamheshimu kwa kutambua kuwa kuna mambo makubwa kuliko madaraka, umaarufu na fedha na hivyo ndivyo tunapaswa kuishi navyo kama muda wetu, nguvu na rasilimali,” amesema Mkapa