Mke wa Kisena kuunganishwa na mumewe Aprili 30

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeshindwa kumuunganisha Florencia Membe, katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mumewe, Robert Kisena, kwa kile ilichoelezwa na upande wa mashtaka kuwa  haujakamilisha uandaaji hati mpya ya mashtaka

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeshindwa kumuunganisha Florencia Membe katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mumewe, Robert Kisena, kwa kile ilichoelezwa na upande wa mashtaka kuwa haujakamilisha uandaaji hati mpya ya mashtaka.

Robert Kisena ambaye ni Mkurugenzi wa  Kampuni ya Huduma za Usafirishaji wa Mabasi yaendayo Haraka  (Udart) na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka 19 yakiwamo ya kutakatisha fedha.

Kwa upande wake, Florencia ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Zenon Oil Gas Limited, anakabiliwa na mashtaka saba likiwamo la kuisababishia hasara ya Sh2.4 bilioni kampuni ya Udart.

Mahakama hiyo imeshindwa kumuunganisha Florencia katika kesi ya uhujumu uchumi namba 11/2019 inayomkabili mumewe na wenzake, kutokana na  upande wa mashtaka kutokukamilisha uandaaji hati mpya ya mashtaka.

Wakili wa Serikali, Wankyo Simon, amedai kuwa wameshindwa kumuunganisha mshtakiwa huyo kwa kile kilichoelezwa kuwa hawajakamilisha kuandaa hati mpya ya mashtaka.

Simon ameeleza hayo jana Jumanne Aprili 23, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, wakati kesi hiyo ilipotajwa.

“Upelelezi wa shauri hili haujakamilika, kesi hii ilikuja kwa ajili ya Florencia kuunganishwa katika kesi inayomkabili mumewe, lakini kwa bahati mbaya  hatujakamilisha kuandaa hati ya mashtaka, hivyo tunaiomba kumuunganisha mshtakiwa huyu Aprili 30 mwaka huu kesi hii itakapokuja kutajwa” amedai Simon.

Hakimu Simba alikubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Aprili 30 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa.

Mbali na Kisena, washtakiwa wengine ni Kulwa Kisena, mhasibu wa kampuni hiyo, Charles Selemani na raia wa China, Chen Shi.

Hata hivyo, mshtakiwa Robert Kisena na Chen Shi hawakuwapo mahakama jana kwa kile kilichoelezwa kuwa ni wagonjwa.

Kati ya mashtaka hayo 19 yanayowakabili washtakiwa hao; moja ni kuongoza mtandao wa uhalifu; manne ya kughushi nyaraka; manne ya  kuwasilisha nyaraka za uongo na manne ya utakatishaji zaidi ya Sh2.4 bilioni.

Mashtaka mengine ni kujenga kituo cha mafuta bila kibali kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) na kuuza mafuta mahali pasiporuhusiwa (makao makuu ya kampuni hiyo - Jangwani).

Mashtaka mengine ni kujipatia zaidi ya Sh1.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu; kuisababishia Udart hasara ya zaidi Sh2.4 bilioni; na wizi wa mafuta yenye thamani ya zaidi ya Sh1.2 bilioni mali ya Udart.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Januari mosi 2011 na Mei 2018, katika ofisi za kampuni hiyo zilizopo eneo la Jangwani, wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam.