Mkono wa sweta hili jingine linawahusu

Tuesday February 12 2019

By Janeth Joseph, Mwananchi [email protected]

Moshi. Baada ya kutajwa kuhusika katika maambukizi ya Ukimwi, wanaume wasiofanyiwa tohara maarufu mkono wa sweta sasa wanaelezwa pia kuwa chanzo cha maambukizi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake.

Hayo yalisemwa na daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Dk Bariki Mchome wakati wa maadhimisho ya siku ya saratani duniani yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.

Dk Mchome alisema saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake ndiyo inayoongoza kusababisha vifo. “Zipo sababu nyingi za mtu kupata saratani ya shingo ya kizazi, asilimia 90 inasababishwa na kirusi kinachoitwa Humani papilloma Virus kama mwanamke atajamiiana na mwanaume ambaye hajatahiriwa ni rahisi kupata kirusi hicho, takwimu zinaonyesha ni hatari,” alisema Dk Mchome na kuongeza: “Ukishafikisha miaka 30 ni vyema ukapime afya, ukiwahi ugonjwa wa saratani unatibika mara nyingi watu wanakuja KCMC wakiwa hatua za mwisho.”

Naye mkurugenzi mtendaji wa KCMC, Dk Gileard Masenga alisema saratani inatibika iwapo mgonjwa atagundulika mapema.

Alisema kati ya mwaka 2016 na 2018 hospitali hiyo ilihudumia wagonjwa 9,312 kati yao 1,445 ni wapya.

Advertisement