Mkulima asimulia jinsi anavyousaka umilionea kwenye zao la mpunga

Ukimsikiliza dakika tano tu anaweza kuwa darasa linaloweza kubadili maisha yako kupitia zao la mpunga. Ni mwanamke jasiri, mhamasishaji na mwenye ndoto za kuwa milionea kupitia kilimo.

Namzungumzia Veronika Urio, au maarufu kwa jina la Mama Vero ambaye ni mkazi wa kijiji cha Wami Dakawa, wilayani Mvomero, mkoani Morogoro anayemiliki ekari 15 za mpunga kwa zaidi ya miaka 17 sasa.

Mama Vero kutoka Chama cha Ushirika cha Uwawakuda kijijini hapo alikuwa kivutio cha mamia ya washiriki wa Mwananchi Jukwaa la Fikra usiku wa Mei 23, mwaka huu katika Ukumbi wa Kisenga, uliopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Jukwaa hilo katika awamu ya nne kupitia mada isemayo ‘Kilimo, Maisha Yetu’, limefanyika ikiwa ni takribani miezi 11 tangu kufanyika jukwaa la kwanza Juni 28 ,2018, chini ya mada kuu ya ‘Afya Yetu, Mtaji Wetu.

Awamu ya pili jukwaa hilo lilifanyika Oktoba 4, 2018 likiwa na mada ya Fursa na Changamoto Kuelekea Uchumi wa Viwanda kabla ya kufuatiwa na awamu ya tatu Februari 7, 2019 likiwa na mada ya Mkaa, Uchumi na Mazingira Yetu.

Akizungumza mbele ya mamia ya washiriki wa jukwaa hilo katika awamu ya nne, Mama Vero ambaye elimu yake ni ya darasa la saba anaamini rasilimali fedha haitakuwa na matokeo chanya kwa mkulima asiyekuwa na hali ya kujituma, uvumilivu na kujifunza kila wakati.

“Ni kazi bure ukipewa fedha bila kuwa na hali ya kujituma mwenyewe. Kwa sababu utapewa fedha na NMB, CRDB, au Benki ya Maendeleo Kilimo (TADB), lakini usipojipanga kama ni mwanamke utanunua vitenge, mwanaume utaoa mwanamke wa pili,” anasema Mama Vero aliyetoa changamoto kwa vijana waliohitimu vyuo vikuu nchini.

Uvumilivu, kutafuta maarifa

Kupitia jukwaa hilo, Mama Vero anaweka wazi hisia zake juu ya ukombozi wa kifikra alioupata kupitia Shirika la Misaada ya Kimataifa la Marekani (USAID) kati ya mwaka 2011/13.

Veronika anasema kabla ya kuanza kilimo cha kisasa kupitia zao hilo, hakuona faida kwa zaidi ya miaka kumi. “Kwa sasa nina miaka 15 katika zao hilo, mwanzoni nilikuwa napata gunia nane hadi tisa tu lakini baada ya kupata mafunzo ya watalaamu wa USAID, kwa sasa ninapata gunia 37 hadi 50 za mpunga katika ekari moja,” anasema Mama Vero.

Akizungumzia kuhusu matokeo chanya ya mafunzo aliyopata, Mama Vero anasema katika mashamba ya Dakawa wakulima walijenga mazoea ya kilimo cha kubahatisha bila kujua ni kiwango gani cha mazao yatapatikana baada ya kupanda mpunga.

“Lakini tulifundishwa tupande kwa sentimita 30, 20 hadi 15, inategemea ni season (msimu) gani, mpunga unahitaji joto, ukipanda februari inabidi utumie sentimita 30, ukipanda mbegu bora kwa umakini utavuna mpunga mwingi,” anasema Mama Vero.

Mafanikio yake

Akizungumza mafanikio yake, Mama Vero anasema USAID imemtoa katika maisha ya ufukara aliyoishi ndani ya miaka 10 bila kuona matunda yoyote katika kilimo cha mpunga, akisema uvumilivu na kutafuta maarifa zaidi ya kilimo cha kisasa ni msingi wa hatua aliyofikia.

Anasema mwaka 2014, alitunukiwa tuzo ya mkulima bora kijijini hapo na USAID, baada ya kuibuka mwanafunzi bora aliyefanikiwa kukuza uzalishaji wake kupitia mafunzo ya USAID ‘feed the future’.

“USAID kwa sasa wamenifanya nikanunua gari, nikajenga nyumba bora, nina chakula kwenye kaya yangu cha mwaka mzima hadi akiba ya mwaka ujao.

Mama Vero mwenye familia na mume ambaye pia ni mkulima wa mpunga kwa sasa ni mkulima anayetumika kama mfano wa kuigwa kupitia Chama cha Ushirika cha Uwawakuda, kijijini hapo.

USAID ilianzisha mpango huo ili kukabiliana na kiini cha njaa katika nchi mbalimbali duniani, ikiwezesha mbinu za uzalishaji wa kisasa.

“Kwa bahati nzuri nilijitoa kama kafara, Watanzania tuna tabia ya kusema haiwezekani, haiwezekani, lakini inawezekana endapo ukiwa na nia vinginevyo hautaweza hata kama utawezeshwa mkopo wa Sh100milioni. Itakuwa ni kazi bure, kazi bure tu.”

“Zamani niliamini profesa wa chuo kikuu tu ndiyo anaweza lakini kumbe hata mimi darasa la saba ninaweza.”

Kilio chake

Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano, Mama Vero anatumia nafasi hiyo kutuma ujumbe kwa Serikali ya mkoa wa Morogoro kuangalia changamoto wanazopata wakulima wa kijiji cha Wami Dakawa.

Mama Vero anasema wakulima wa mpunga wanakabiliwa na changamoto ya mitaji kwa ajili ya kuongeza uzalishaji.

Pamoja na changamoto hiyo, anasema maofisa wa kilimo kijijini hapo wamekuwa kikwazo.

“Kazi yao ni kukatisha tamaa tu wakulima, tunaomba Serikali ya mkoa itusaidie kwa hilo,”anasema Mama Vero ambaye kwa sasa ni mkufunzi wa kilimo cha kisasa cha mpunga.