Mkurugenzi LHRC akwaa tuzo ujasiri

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, akionyesha Tuzo ya Kimataifa ya Mwanamke Jasiri kwa mwaka 2019 baada ya kukabidhiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo (kushot) na Mke wa Rais wa Marekani Melania Trump juzi jijini Washington D.C. Anna Henga anakuwa ni Mtanzania wa pili kutunukiwa Tuzo ya Kimataifa ya Mwanamke Jasiri, akifuata nyayo za Vicky Ntetema aliyepata tuzo hii mwaka 2016. Picha Ubalozi wa Marekani

Muktasari:

  • Katika hafla hiyo, Pompeo alisisitiza umuhimu wa kuheshimu na kutambua ujasiri na jitihada za wanawake wanaojitoa kwa ajili ya kuhudumia na kusaidia jamii zao.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga ameshinda tuzo ya Mwanamke Jasiri akiwa ni miongoni mwa wanawake 10 duniani waliotunukiwa tuzo hiyo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo.

Kwa kujibu wa taarifa iliyotolewa katika tovuti ya ubalozi wa Marekani nchini, Henga anakuwa mwanamke Mtanzania wa pili kupokea tuzo hiyo, wa kwanza alikuwa Vicky Ntetema ambaye alitunukiwa mwaka 2016.

Taarifa hiyo imeeleza kwamba, Henga amejitoa katika taaluma yake kupigania haki za binadamu hapa nchini akijikita zaidi kwa wanawake na watoto na kwamba jitihada hizo zilidhihirika Machi 7 mjini Washington alipotunukiwa tuzo hiyo mbele ya Melania Trump, mke wa Rais wa Marekani, Donald Trump.

Huu ni mwaka wa 13 tangu Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilipoanza kutoa tuzo hiyo kwa wanawake jasiri wenye mchango kwenye jamii zao. Tangu tuzo hizo zilipoanza kutolewa Machi 2007, wanawake 120 kutoka nchi 65 tofauti wametambuliwa na kutunukiwa tuzo hiyo.

Katika hafla hiyo, Pompeo alisisitiza umuhimu wa kuheshimu na kutambua ujasiri na jitihada za wanawake wanaojitoa kwa ajili ya kuhudumia na kusaidia jamii zao.

“Wanawake jasiri wako kila mahali. Wengi wao hawaheshimiwi. Wanakabiliwa na changamoto nyingi, changamoto tunazozikabili. Wanawake jasiri wako kila mahali na wanahitajika kila mahali,” alisema Pompeo.

Wanawake wengine tisa waliotunukiwa tuzo hiyo wanatoka katika mataifa ya Bangladesh, Burma, Djibouti, Egypt, Jordan, Ireland, Montenegro, Peru na Sri Lanka.

Hafla ya utoaji tuzo hizo ilikuwa wazi kwa vyombo vya habari na ilirushwa moja kwa moja kupitia tovuti ya Ikulu ya Marekani.

Tuzo hiyo ilianzishwa mwaka 2007 kwa lengo la kutambua mchango wa wanawake wanaojitoa kwa nguvu na ujasiri kama viongozi katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii zao bila kujali hatari ya maisha yao binafsi.

Mpaka sasa kupitia tuzo hiyo, Ikulu ya Marekani imetambua mchango wa wanawake zaidi ya 120 kutoka nchi zaidi ya 65 katika kutetea haki za binadamu, kudumisha nafasi ya wanawake katika jamii na kudumisha amani na utawala bora katika nchi zao.