Mkurugenzi Mtendaji Vodacom, wafanyakazi kadhaa mikononi mwa polisi

Hisham Hendi 

Muktasari:

Wafanyakazi hao wa Vodacom wafanyakazi hao wanahojiwa kuhusiana na matumizi mabaya ya rasilimali za mtandao huo.


Dar es Salaam. Siku chache baada ya kuthibitishwa, mkurugenzi mtendaji, Hisham Hendi pamoja na wafanyakazi kadhaa wa kampuni ya Vodacom wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo leo, Aprili 3, wafanyakazi hao wanahojiwa kuhusiana na matumizi mabaya ya rasilimali za mtandao huo.

“Vodacom itaendelea kutoa ushirikiano kwa mamlaka za usimamizi. Tumewaambia wafanyakazi wetu watafikishwa mahakamani na kupandishwa kizimbani leo (Aprili 3) ingawa hakuna kesi iliyofunguliwa dhidi yao mpaka sasa,” imesomeka sehemu ya taarifa iliyotolewa na Vodacom.

Baada ya kukaimu nafasi hiyo kwa mezi tisa, Hendi alithibitishwa kuwa mkurugenzi mtendaji wa Vodacom Tanzania tarehe 19 ya mwezi uliopita akichukua nafasi ya Ian Ferrao aliyemaliza mkataba wake Juni mwaka jana. 

Vodacom imesema mahojiano hayo hayataathiri huduma zake kwa namna yoyote hivyo wasiwe na wasiwasi kwani watalaamu waliopo wanatosha kushughulikia kila kitu.

“Tutaendelea kuwajuza kitakachoendelea,” imesema kampuni hiyo yenye wateja zaidi ya milioni 14 wa simu za mkononi.