Mkurugenzi amjaribu Magufuli uvumilivu

Musoma. Wakati Rais John Magufuli akiwataka wateule wake kuwa na ushirikiano badala ya kuwa na misuguano baina yao, hali hiyo imeendelea mkoani Mara ambapo kumetokea majibizano kati ya katibu tawala wa mkoa huo, Carolina Mthapula na mmoja wa wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo.

Hali hiyo imefichuliwa mjini hapa juzi na mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima katika hafla ya kumwapisha mkuu mpya wa wilaya ya Tarime, Charles Kabeho ambapo alisema majibazano hayo yametokea baada ya katibu tawala huyo kumuandikia barua ya onyo mkurugenzi huyo ambaye hata hivyo hakumtaja jina.

“Nimepewa barua ya page (kurasa) nane aliyoandika mkurugenzi huyu akimjibu Ras (katibu tawala) tena anamwambia kuwa ‘huna mamlaka ya kunipangia cha kufanya kwavile sote tumeteuliwa na Rais’ nikajiuliza mara mbili mbili huyu mkurugezni ana akili kweli” alisema Malima.

Malima alisema kabla ya mkurugezi huyo kutoa majibu hayo, katibu tawala huyo alimwandikia barua ya onyo juu ya tabia yake ya ulevi na kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wake za watu huku akiwadhalilisha wanawake kwa kuwashikashika kwenye baa akimueleza kuwa tabia hiyo haiendani na maadili ya kazi na kwamba inadhalilisha nafasi yake.

Akizungumza baada ya kuapishwa, Kabeho alisema mbali na kudhamiria kuleta maendeleo kwa wananchi wa wilaya hiyo, pia atahakikisha migogoro iliyodumu kwa muda mrefu inapatiwa ufumbuzi.