Mkuu wa Majeshi Mabeyo asisitiza umakini katika kulitegemeza Kanisa Katoliki

Muktasari:

Mgeni rasmi katika sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Halmashauri ya Walei nchini, CDF Venance Mabeyo amebainisha changamoto mbalimbali zinazowakabili walei katika kipindi hicho ikiwa ni pamoja na waumini kutoelimishwa juu ya michango wanayotoa kulitegemeza kanisa.

Dar es Salaam. Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Venance Mabeyo amesema dhana ya kulitegemeza Kanisa inatakiwa kufanyika kwa umakini ili lsiathiri shughuli za kiroho za Kanisa Katoliki.

Mabeyo ameyasema hayo leo Jumapili Juni 16, kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya Halmashauri ya Walei iliyoongozwa na Kardinali Polycarp Pengo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro, Kamishna wa Uhamiaji, Anna Makakala, Spika mstaafu, Anna Makinda na Rais mstaafu wa Bunge la Afrika, Getrude Mongela.

Amesema jambo hilo liwe ni la kiimani zaidi na muumini afundishwe kwanini anatakiwa kutoa na asipotoa maana yake ni nini. Amesema hilo litasaidia kuendelea kukuza imani za waumini wa kanisa hilo kwa kufanya wanachokijua.

“Mambo haya yafanyike kwa umakini zaidi ili isionekane Kanisa linapigia chapuo mambo ya fedha kuliko imani,” amesema Mabeyo ambaye ameambatana na mkewe, Tina Mabeyo pamoja na watoto wao.

Sherehe za maadhimisho hayo zimehudhuriwa na mamia ya waumini pamoja na maaskofu wote wa Kanisa Katoliki nchini, mapadri na wawakilishi wa halmashauri za walei kutoka majimboni.