Mkuu wa mkoa asaka wanaotumia jina lake kutoa zabuni

Wednesday January 9 2019

 

By Hawa Mathias, Mwananchi [email protected] mwananchi.co.tz.

Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amewaonya watumishi wa Serikali wanaotumia jina lake vibaya wakati wa utoaji wa zabuni za miradi ya mbalimbali ya maendeleo na kuwataka makandarasi wazawa kutoa taarifa za siri ili wabanwe.

Chalamila alitoa kauli hiyo jana alipofanya mkutano na makandarasi wa ndani wa kusikiliza kero zao, ikiwemo ya kukithiri kwa rushwa na ukiritimba wakati wa utoaji wa zabuni hasa za barabara na maji.

Alisema kuwa amepata taarifa za baadhi ya watumishi kutumia jina lake vibaya na kudiriki kuwaeleza watu wanaoomba zabuni kutoa kiasi fulani cha fedha kwa madai kuwa amewatuma kufanya hivyo.

Awali, Rais wa Makandarasi Wazawa Tanzania, Kura Mayuma alimuomba Chalamila kuwamulika watumishi wa umma wanaotoa zabuni katika ofisi yake kwa sababu wanaonyesha dalili za kutaka kupokea rushwa ili watoe kazi.

Mwenyekiti wa Umoja wa Chama cha Makandarasi Tanzania (Cata) Mkoa wa Mbeya, Salum Ndauka alisema baadhi ya viongozi wa Serikali wamekuwa wakiwadhalilisha kwa kuwakamata na kuwafikisha polisi pindi miradi inapokuwa haijakamilika.

Advertisement