Mkwasa: Mungu tu amependa niendelee kuishi

Kwa Tanzania, ni nadra kwa mchezaji kuitumikia klabu fulani na kisha kuwa kocha na baadaye kiongozi. Iko hivyo lakini kwa wachache imetokea.

Spoti Mikiki limefanya mahojiano na Charles Boniface Mkwasa aliyefanya yote Yanga, mchezaji, kocha na baadaye kiongozi na zaidi akieleza hatua yake ya kuumwa na kutema kibarua klabuni hapo. Fuatana naye.

“Ilikuwa Jumapili tuko kanisani tumesimama kuimba, niliishiwa nguvu, sikuweza kuendelea kusimama, Betty, mke wangu alikuwa jirani akaniambia kaa chini, nilikaa hadi ibada ilipokwisha. Mwili haukuwa na nguvu kabisa,” ndivyo ambavyo mchezaji, kocha na katibu mkuu wa zamani wa Yanga anasimulia.

Anasema tukio lililomtokea kanisani lilikuwa ni muendelezo wa dalili ambazo alikutana nazo mara kwa mara lakini hakuzipa uzito sana, lakini Mungu alipenda aendelee kuishi kwani kama sio kushtuka na kutafuta tiba mapema kwani anasema kama si hivyo basi sasa hivi angekuwa ameshahaulika.

“Nilitokewa na dalili nyingi mno, lakini sikutilia maanani sana kuwa ni tatizo kubwa, nilihisi labda umri, kuna wakati nilihisi baridi sana, kipindi kingine joto kali, niliishiwa nguvu, nilikosa hamu ya kula na kuchoka kupita kupita kiasi, mwishoni nikajikuta hadi kumbukumbu zinapotea na sauti kukauka,” anasimulia

Anasema wakati dalili hizo zinamtokea, alihisi joto ni hali ya hewa ya Dar es Salaam, dalili ya kuchoka alihisi amefanya kazi nyingi na umri kusogea, hakuwahi kufikiria kama dalili hizo ni za ugonjwa hatari ambao kama angechelewa kidogo tu kwa mujibu wa madaktari, basi yangekuwa mengine.

Mambo yalianza akiwa Mtendaji Yanga

Anasema kuna wakati alipokuwa Katibu Mkuu wa Yanga, akiwa ofisini Yanga, anaweza kuwa anafanya kitu fulani, lakini ghafla akasahau, kama alikuwa anaandika barua fulani, ghafla tu anasahau, akikumbuka tayari siku imepita, wakati mwingine kama alipaswa kuelekea kazini saa moja asubuhi, basi anajikuta amechoka na kukaa nyumbani hadi saa tatu asubuhi ndipo anakwenda.

“Nikirudi nyumbani nako ilikuwa ni vivyo hivyo, kama nimekuta chakula hakipo mezani, basi napitiliza chumbani, nikiitwa kuja kula naweza nikaa hata saa nzima tangu nimeitwa kwenye chakula ndipo nakwenda, yaani nilikuwa na matukio ambayo sikujua chanzo chake.

Anasema aliamua kwenda kupima akihisi ni maralia au uchovu, lakini siku familia ikamshauri kwenda kwenye moja ya hospitali ya binafsi ambayo ni kubwa tu hapa Dar es Salaam, ambako alitibiwa na kuambiwa ana tatizo kwenye moyo.

“Nilimpigia profesa Janabi (Mohammed ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo yA JKCI) yule ni ‘family friend’ wetu, nikamueleza akaniambia ratiba yake ya wagonjwa atapata nafasi ndani ya mwezi mmoja na nusu, hivyo nisubiri hapo katikati atanicheki.

“Nikatoka kwenda kwa daktari mmoja anaitwa Dk Masatu yuko Labinsia hopitali, nikafanyiwa vipimo tena, majibu yalipokuja nilikuwa niko na Dk Masatu tunaongea tu kama kawaida, alivyoviona akabadilika.

“Ilionyesha tatizo langu ni kubwa kidogo, niliambiwa baadhi ya mishipa ya damu kwenye moyo imeziba, sikuwa na namna pale pale nilipata wazo la kwenda India, nilimpigia tena Profesa Janabi nikamueleza akakubaliana na mpango huo,” anasimulia.

ALIVYOAJIUZULU YANGA

Mkwasa anasema, akiwa katika harakati za kuhakikisha afya yake inarejea, ndipo wakati mwuafaka ambao aliona sasa aondoke Yanga.

“Nilifikiria kuomba likizo ya ugonjwa, lakini nikaona hiyo itasababisha watu kuongea maneno maneno, nikaona bora niondoke moja kwa moja kwenye masuala ya mpira, nipumzike.

“Nilikaa mwenyewe, hakuna aliyenishauri niandike barua, nilifanya uamuzi binafsi, lakini nikiishirikisha familia yangu,” anasema.

Anasema baada ya kuandika barua ya kujiuzuru, kwa kiasi fulani aliona kama ametua mzigo kichwani, hakujua ni kwa sababu gani lakini tangu pale alijiona ametua mzigo.

“Nilimpigia simu profesa Janabi nikamwambia dokta leo kama najiona kichwa changu chepesi, akaniuliza kwanini nikamueleza kuwa ni baada ya kujiuzulu Yanga, Profesa akaniambia, huo ni mzigo namba moja, hongera kwa uamuzi uliochukua.

MIPANGO YA INDIA YAANZA

Mkwasa anasema, baada ya hatua hiyo, harakati za kwenda India kwenye matibabu zilianza, ambapo alipewa mawasiliano ya hospitali kama nne za kule na kuchagua mojawapo.

“Tuliwasiliana nao, kiukweli wako fasta mno katika kujibu na kwa kuwa ilikuwa ni safari ya ghafla, gharama za ndege zilikuwa juu kidogo, kwenda na kurudi kwa mtu mmoja ilikuwa Dola 1400 hivyo mimi na mke wangu ikatugharimu Dola 2800.

“Tulipofika Uwanja wa Ndege kule India alikuja mtu kutupokea, pale hakujua kati yangu na Betty nani mgonjwa, wote tulikuwa tunatembea vizuri tu, tukaenda hotelini, siku iliyofuata tukiwa na mizigo yetu tukahamia hospitali.

Anasema walipofika hospitali, walipokewa vizuri, daktari aliwauliza maswali kujua chanzo cha tatizo kabla ya vipimo kuanza ambapo viligharimu kama Dola 6600 pamoja na matibabu, malazi na chakula na kila kitu pale hospitali.

ILIKUWA NI MUUJIZA TU

Mkwasa anasema alipoanza vipimo aliingizwa kwenye chumba kikubwa ambacho kilikuwa na vifaa hawajawahi kuviona, wakati yeye akifanyiwa vipimo, jopo la madaktari wengine walikuwa chumba kingine wakifuatilia kwenye skrini vipimo vile.

“Majibu ya vipimo yalionyesha kati ya mishipa mitatu kwenye moyo, mmoja uliziba, mwingine nao ulikuwa unaelekea kuziba na mmoja pekee ndiyo ulikuwa unafanya kazi.

“Walishauri kuizibua, nikawauliza hawawezi kuzibua mmoja na ule mwingine ikawa siku nyingine, wasiwasi wangu ilikuwa gharama huenda zingekuwa kubwa kupitiliza, kama walijua wakaniambia wala usiwe na wasiwasi na gharama, nikapangiwa Agosti 4 kuwa siku ya oparesheni.

“Siku hiyo alikuja daktari anaitwa Nilesh, kazi yake ilikuwa ni kunirejesha kwenye saikolojia ya kawaida kabla ya operesheni, aliniambia nimekwenda hospitali wakati muafaka kama ningechelewa kidogo tu yangetokea mengine.

APASULIWA KWA MSUMENO WA UMEME

Anasema alipelekwa chumba cha upasuaji asubuhi na shughuli ilianza saa 3:00 asubuhi ambapo ilikuwa shughuli pevu kiasi kwamba leo hii akiambiwa arudi hawezi.

“Nilipasuliwa na msumeno wa umeme kifuani, hadi jirani na tumbo, moyo wangu ukatolewa ukawekwa kwenye chombo kama kina barafu, halafu mimi nikawekewa mashine ya mfano wa moyo kwa ajili ya kunisaidia.

“Nilitobolewa matundu matatu tumboni, moja la kuingiza maji, hewa na damu, na ubavu wa kulia waliingiza walitoa tundu jingine na kuweka mpira wa kutoa maji na tundu jingine lilikuwa shingoni.

“Walinichana miguu yote miwili na kutoa mishipa miwili na mkono wa kushoto walinichana na kutoa mshipa mmoja hivyo ikatimia ile mitatu ambayo waliniwekea kwenye moyo.

“Kwenye mkono walinishona na kitu kama stepla ambapo wakati wanashona ni kama mtu anabana kitu na stepla, baada ya oparesheni, ile mipira niliyowekewa baada ya kutobolewa waliika vikabaki vipisi ambavyo vilitolewa baada ya siku mbili.

Anasema siku vipisi hivyo vya mipira vinatolewa, maumivu yake hatokaa hayasahau kwani vipisi vile vilivutwa na kutolewa bila ganzi, lakini ndiyo ilikuwa kupona kwake.

“Niliambiwa mishipa niliyotolewa miguuni na mkono wa kushoto itarudi lakini baada ya mwaka mmoja, lakini pia niliambiwa nitarudi katika hali yangu ya kawaida taratibu na kumbukumbu pia zitaanza kurejea taratibu baada ya wiki moja.

“Lakini hata wao walishangaa baada ya saa kadhaa mimi kumbukumbu zilianza kurejea, hiyo ni kutokana na historia ya maisha yangu, nimekuwa mwanamichezo na nina utaratibu wa kufanya mazoezi, kitu ambacho hata mke wangu Betty na wanangu wanakifanya kila siku.

MIPANGO YAKE KURUDI YANGA IKOJE

Mkwasa anasema madaktari kule India wamemtaka arudi tena kliniki mwezi Mei, baada ya pale sasa ataruhusiwa kuendelea na shughuli zake hata akitaka kucheza mpira ataweza.

“Kipaumbele changu baada ya kupona ni kuendelea na kazi yangu ya ukocha, hiyo ndiyo naifikiria, kurudi kwenye uongozi, sitarajii sana na si mipango yangu.”