Mlinga ashangaa wazinifu kupewa kondomu bure

Mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga

Muktasari:

Mbunge wa Ulanga, Godluck Mlinga amesema inamshangaza kuona Serikali inawajali wazinifu huku wanafunzi wa kike wakiachwa wakishindwa kupata taulo za kike.

Dodoma. Serikali imetakiwa kuwasaidia wanafunzi wa kike kupata taulo za kike kwa umuhimu wake kwani imeweza kuwasaidia wazinifu kwa kugawa mipira ya kiume (kondomu) bure kwa nini ishindwe kwa watoto wa kike.

Mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga ameuliza swali hilo leo bungeni Jumatano Mei 22, 2019 ambapo ameshangazwa na utaratibu wa Serikali kuwapa kipaumbele watu aliosema ni wazinifu.

Mlinga amesema wanafunzi wa kike wanashindwa kufanya vizuri katika masomo yao kutokana na kutumia muda mwingi kuwa nyumbani huku wengine wakiendelea na masomo yao.

"Bei za vitu vingi zimepunguzwa, kama dawa na mambo mengine, lakini huko mitaani Serikali inagawa kondomu bure huku ikishindwa kugawa bure taulo za kike kwa wanafunzi, je Serikali inatoa kipaumbele kwa wazinifu kuliko watoto wa kike?" Amehoji Mlinga.

Wabunge wengi wakiongozwa na Margaret Sitta walimshangilia kwa kugonga meza zaidi huku wengine wakimfuata na kumpa mkono kama sehemu ya kutambua mchango wake.

Spika Job Ndugai amesema Serikali imesikia kilio cha mbunge huyo na italifanyia kazi jambo hilo.