Mmiliki wa facebook azishauri Serikali kuweka sheria

Muktasari:

  • Sheria hizi mpya zinapaswa kuwa sawa katika tovuti zote,   ili iwe rahisi kuzuia taarifa za kudhuru zisisambae haraka kwenye mitandao yote

Washington,Marekani. Mmiliki wa Mtandao wa Kijamii wa Facebook, Mark Zuckerberg amezitaka serikali kote ulimwenguni kusaidia kuweka sheria za udhibiti wa taarifa za intaneti.

Zuckerberg ameandika barua ya wazi akitoa wito sheria ziwekwe ili kufuatilia taarifa za intaneti.

Katika waraka wake wa wazi uliochapishwa na gazeti la Washington Post  anasema jukumu la ufuatiliaji wa maudhui hatari ni kubwa sana kwa kampuni ya Facebook.

Wito wa mmiliki huyo wa Facebook unakuja wiki mbili baada ya mtu mwenye silaha kutumia mtandao huo kusambaza video yake moja alipokuwa akiushambulia msikiti eneo la Christchurch, New Zealand.

"Watunga sheria mara nyingi huniambia tuna mamlaka makubwa juu ya kauli, na kusema ukweli ninakubaliana,"  Zuckerberg ameandika na kuongeza kuwa Facebook inabuni bodi huru ili watu waweze kukata rufaa juu ya uamuzi mbalimbali juu ya kile kinachotumwa na kile kinachoondolewa kwenye mtandao huo.

Anaelezea mpango mpya wa kuweka sheria kama mfumo ambao angependa kuona unatekelezwa na kampuni nyingine  pia za teknolojia.

Anasema ziwepo sheria za pamoja ambazo mitandao yote ya habari ya kijamii inahitaji kufuata, kudhibiti kutekelezwa na kampuni nyingine, kudhibiti kusambaa kwa taarifa za zinazosababisha madhara.

Pia, ameshauri kampuni zote za teknolojia kutoa ripoti ya wazi kila baada ya miezi mitatu, sawia na ripoti yao ya fedha.

Ameshauri sheria kali ziwekwe kote duniani kulinda maadili ya uchaguzi na kuwapo kwa viwango sawa kwa tovuti zote za kuwatambua wanasiasa.