Mnyeti aagiza kuanzishwa vituo vya kuuza madini

Mkuu wa mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti

Muktasari:

 

 

  • Katika utekelezaji maagizo ya Rais John Magufuli kuhusu soko la madini, mkuu wa mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti ameagiza kuanzishwa vituo vya ununuzi wa madini katika wilaya zenye madini ili kurahisisha biashara na Serikali kupata kodi.

Babati. Mkuu wa mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti ameagiza vituo vya ununuzi wa madini vijengwe kwenye wilaya zenye madini ili kurahisisha soko la madini kwa wachimbaji.

Mnyeti aliyasema hayo jana Jumamosi Februari 2, 2019 wakati akizungumza na wadau wa madini mjini Babati mkoani humo kwenye kikao cha kupitia rasimu ya kanuni za masoko ya madini.

Mnyeti alisema kituo cha ununuzi wa madini ya Tanzanite kimeshajengwa mji mdogo wa Mirerani hivyo na maeneo mengine ya madini nayo yajenge vituo vya madini.

Alisema vituo hivyo vitakuwa na huduma zote muhimu zikiwemo taasisi za fedha na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kurahisisha biashara ya madini kufanyika.

Ofisa madini Simanjiro, Daudi Ntalima alisema wanapokea maoni ya rasimu hiyo yenye mapendekezo mbalimbali ili kuiwasilisha serikalini.

Alisema mnunuzi atanunua madini kwa kuzingatia taarifa za madini yaliyopo ghalani na iwapo atahitaji kuona madini ataruhusiwa kwa utaratibu ulioandaliwa.

"Tume ya madini itaweka bei elekezi ya madini katika soko hili na hivyo hakuna mnunuaji atakayeweza kununua madini chini ya bei elekezi," alisema Ntalima.

Mwenyekiti wa sekta ya madini ya Tanzanite, Money Yousuph alisema kwamba mapendekezo hayo yana baadhi ya vipengele vinavyowabana wadau wa madini.

Yousuph alisema kwamba mchimbaji akipata madini yake anapaswa kuwa nayo ili akiamua ayauze au ayaweke kwa ajili ya maonyesho, itakuwa ni uamuzi wake.

Makamu mwenyekiti wa kamati ya usalama migodini, afya na mazingira wa shirikisho la wachimbaji madini nchini (Femata) Dokta Bernard Joseph alisema kanuni hizo zikipitishwa wadau watanung'unika pembeni. 

Ofisi madini mkoa wa Manyara, Joseph Kumburu aliyataja baadhi ya madini yanayopatikana mkoani humo kuwa ni Tanzanite, dhahabu, tomarin, rubby na emerald.

Mhandisi Kumburu alisema Tanzanite ipo Mirerani, rubby inapatikana Kiteto na Simanjiro, emerald ipo Babati, chumvi ipo Hanang' na dhahabu inapatikana Mbulu pamoja na Kiteto.