Mnyika adai wanajeshi wamechoma, kubomoa nyumba za wananchi Dar

Muktasari:

  • Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika ametaka idhini ya Spika, Job Ndugai kutoa hoja bungeni juu ya wanajeshi kubomoa na kuchoma nyumba katika mitaa ya Kisokwa na Mlongazila wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam.

Dodoma. Mbunge wa Kibamba (Chadema),  John Mnyika amesema mamia ya wakazi wa mitaa ya Mlongazila na Kisokwa jijini Dar es Salaam wanalala nje kutokana na wanajeshi kuchoma moto na kubomoa nyumba zao.

Mnyika ameomba mwongozo bungeni leo Ijumaa Mei 3 kwa kutumia kanuni ya 47 akiomba idhini ya kutoa hoja juu ya jambo la dharura lenye maslahi kwa umma.

“Kuanzia jana katika mtaa wa Kisokwa na Mlongazila mitaa ambayo inabishaniwa kati ya manispaa ya Ubungo na Kisarawe iko upande upi kumetokea jambo lililofanywa na Jeshi la Wananchi (JWTZ),” amesema.

Amesema tukio hilo limehusisha kuchoma moto na kuvunja nyumba za wananchi na kwamba kuna wananchi ambao wamelala nje ya nyumba.

“Sasa jambo hilo ni la dharura kwa sababu ya bomoabomoa hiyo na uchomaji wa nyumba bado unaendelea hivi sasa wananchi wanaendelea kuathirika,” amesema Mnyika.

Amemuomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuagiza kusitishwa kwa bomoabomoa na uchomaji wa nyumba na kuwatuma mawaziri watatu kutatua mgogoro huo.

Amewataja mawaziri watakaounda timu hiyo kuwa ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi; Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo na Waziri wa Ulinzi na Jeshi ka Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi.

Amesema hakukuwa na mgogoro kati ya wananchi na JWTZ lakini kulikuwa ulipaji wa fidia ili kupisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).

Amesema tayari tathimini ya mali hizo ilishafanyika lakini wakati wakisubiri kulipwa fidia kumetokea uvamizi huo.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu,  Jenista Mhagama amesema jambo hilo ndiyo Serikali imelipata na kwamba kwakuwa anasema inahusisha wizara tatu anaomba waachiwe muda waweze kufuatilia.

“Mjadala hapa ndani utatulazimu Serikali tuweze kutoa majibu yetu ni lazima tuwe katika position (nafasi) kulifahamu vizuri na kulitolea ufafanuzi. Tunaomba utuachie tufuatilie na kujua kiini na kama utaona inakupendeza tutakurudishia majibu,” amesema.

Akijibu mwongozo huo, Spika Job Ndugai  amesema kwa uhakika ndiyo wanasikia jambo hilo na hivyo ni vyema Serikali kuachiwa iweze kulitolea ufafanuzi.

“Ni vizuri tuwaachie wenzetu kwa mapendekezo uliyoyatoa ili waweze kuyafanyia kazi kwa wakati muafaka tutaona way forward ya jambo hili ya namna ya kwenda nalo lakini tumelipokea kama meza,” amesema Ndugai.