Mpango ataja sababu kupungua kwa abiria treni ya Mwakyembe

Wabunge wakisoma kitabu cha hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kuhusu hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka wa fedha 2018 na mpango wa maendeleo wa taifa wa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Serikali imesema sababu za kupungua kwa abiria wa treni Mwakyembe ni kuhamishwa kwa kituo kutoka mjini kwenda Kamata kupisha ujenzi wa reli ya kisasa.


Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema abiria wanaotumia treni ya jijini Dar es Salaam imepungua kwa asilimia saba kutokana na kuhamishwa kwa muda kituo cha abiria cha Stesheni ya Dar es Salaam kwenda kituo cha Kamata ili kupisha ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).

Hayo yamesemwa bungeni leo Alhamisi, Juni 13, 2019 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alipokuwa anawasilisha ripoti ya hali ya uchumi kwa mwaka 2018.

Amesema treni hiyo ilisafirisha abiria milioni 5.3 katika umbali wa kilometa 172,239,904 mwaka 2018 ikilinganishwa na abiria milioni 5.7 waliosafiri umbali wa kilometa 185,165,520 mwaka 2017 sawa na upungufu wa asilimia 7.0.

“Upungufu huo ulitokana na kuhamishwa kwa muda kituo cha abiria cha Stesheni kwenda kituo cha Kamata kupisha ujenzi wa reli,” amesema.