VIDEO: Mrithi wa Joshua Nassari aapishwa bungeni

Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia (kushoto) akimpongeza Mbunge mpya wa jimbo la Arumeru Mashariki (CCM), Dk John Pallangyo baada ya kuapishwa bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amemuapisha Dk John Pallangyo kuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki (CCM) akijaza nafasi ya Joshua Nassari (Chadema) aliyepoteza sifa za kuwa mbunge.

Dodoma. Dk John Pallangyo ameapishwa leo Jumatano Mei 22, 2019 kuwa mbunge wa Arumeru Mashariki (CCM) kuchukua nafasi ya Joshua Nassari (Chadema) aliyepoteza sifa za kuwa mbunge.

Dk Pallangyo ameapishwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai huku wabunge wa CCM wakimsindikiza kwa mbwembwe na kuimba nyimbo za CCM,  wakati wakimsindikiza.

Mara baada ya kuapishwa alikwenda kusalimiana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi na Wenye Ulemavu.

Baadaye alihamia upande wanapokaa wapinzani na kusalimiana na Kaimu Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Joseph Selasini na Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika ambao kwa pamoja waliteta kidogo kama sekunde kadhaa.

Kisha mtumishi wa Bunge alimpeleka eneo ambalo atakuwa akikaa.

Dk Pallangyo amechukua nafasi hiyo baada ya Nassari kupoteza fursa hiyo kwa kutohudhuria vikao vya mikutano mitatu ya Bunge mfululizo pasina kutoa taarifa kwa ofisi ya Spika.

Mbunge huyo mpya, alipita bila kupingwa baada ya Chadema kutosimamisha mgombea huku wagombea wa vyama vingine wakienguliwa kwa kukosa sifa za kupitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Tofauti na wabunge waliohama upinzani na kisha kupitishwa na CCM kugombea, walipokuwa wakiapishwa, wabunge wa upinzani walikuwa wakitoka na kutoshuhudia kiapo lakini leo wabunge wa upinzani wamebaki na kushuhudia kiapo hicho.