Mrithi wa Seif CUF leo

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Saba wa CUF wakifuatilia mwenendo wa kikao kabla ya mkutano huo kumalizika jana jijini Dar es Salaam. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  • Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, mkurugenzi wa habari wa CUF, Abdul Kambaya alisema uchaguzi wa kanda ulikamilika jana asubuhi.

Dar es Salaam. Baraza kuu la uongozi la CUF litakutana leo kwa ajili ya kujadili jina la katibu mkuu mpya, uwezekano mkubwa ukiwa ni kutomrudisha Maalim Seif Sharrif Hamad, ambaye ametofautiana na mwenyekiti wake kwa muda mrefu sasa.

Na hilo linawezekana baada ya CUF kupitisha mabadiliko ya katiba siku ya kwanza ya Mkutano Mkuu yanayoondoa katibu mkuu wa kuchaguliwa na kufanya nafasi hiyo iwe ya kuteuliwa, huku mwenyekiti akipewa mamlaka ya kuteua akishirikiana na makamu mwenyekiti wa Bara na Zanzibar.

Hatua hiyo ya CUF imekuja baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa viongozi wa kanda uliofanyika kwa siku tatu mfululizo ili kupata wajumbe wa Baraza Kuu.

Hivyo, katika mkutano wa leo, mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba atawasilisha majina matatu ya nafasi ya katibu mkuu na matatu ya nafasi ya manaibu katibu wakuu Bara na Zanzibar kwa ajili ya kujadiliwa kabla ya kupendekezwa moja kushika nafasi hiyo.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, mkurugenzi wa habari wa CUF, Abdul Kambaya alisema uchaguzi wa kanda ulikamilika jana asubuhi.

Alisema kukamilika kwa uchaguzi huo kunatoa nafasi ya kujulikana kwa wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi.

Alisema baraza hilo ndilo litapokea na kujadili litajadili jina la katibu mkuu.

Alisema baada ya kikao cha baraza watatoa taarifa.

“Kuna uwezekano mkubwa siku hiyo katibu mkuu akawa ameshapatikana kama vikao vitakwenda kama ilivyopangwa,” alisema Kambaya.

“Tumemaliza kupiga kura mapema kabisa, kilicholeta shida ni kura zilizidi ndiyo maana viongozi walikwenda kujifungia kwenye ofisi za makao makuu ya chama kuliweka hilo sawa,” alisema.

Hali ya kutoelewana baina ya Profesa Lipumba na Maalim Seif ilianza mwaka 2016 wakati mwenyekiti huyo aliposema amerejea kwenye kiti chake baada ya kukaa nje kwa takriban mwaka mmoja. Alijivua nyadhifa zake CUF mwaka 2015 wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu, akipinga chama hicho kukubaliana na vyama vingine vinne kumsimamisha Edward Lowassa kugombea urais chini ya mwamvuli wa Ukawa.

Hata hivyo, Maalim Seif alipinga kurejea kwake, akisema alishajiuzulu na hivyo si mwenyekiti tena.