VIDEO: Msako kwa walioghushi fomu za afya shule za bweni kuanza

Monday January 14 2019

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ametoa agizo kwa wakuu wa shule zote za bweni kuhakikisha wanafunzi wamepimwa ili kudhibiti ugonjwa wa kifua kikuu (TB) na kuwataka wazazi kuacha kughushi vyeti.

Katika kufuatilia hilo Waziri Ummy amewaagiza waganga wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha wanafanya ukaguzi katika shule zote za bweni kuhakiki iwapo wanafunzi wamepimwa au lah!

Waziri ameyasema hayo leo Jumatatu Januari 14, 2019 wakati akikabidhi rasmi magari 10 na pikipiki 35 kwa waganga wakuu na waratibu wa mikoa kwa ajili ya kuongeza kasi ya ugunduzi wa ugonjwa wa TB.

“Narudia tena kusisitiza wakuu wa shule za bweni mhakikishe mnafuatilia suala hili na waganga wakuu mpo hapa hakikisheni mnapita katika shule hizi, mhakikishe mnapita kuhakikisha kila mtoto ana cheti cha daktari,” amesema.

Ummy alitoa onyo kwa madaktari kuacha kuchukua fedha kutoka kwa wazazi na kuwaandikia wanafunzi vyeti vya kughushi pasipo kuwapima.

“Watoto wapimwe afya na si kujaziwa tu fomu, kwa sababu fomu za afya zipo mtoto anakwenda pale anajaziwa tu amepimwa, hata wazazi pia waone kuwa hilo ni jukumu lao kwa ajili ya kuwakinga watoto wao na kujua maendeleo yao kiafya,” amesisitiza.

Advertisement