Mtalii anasa kwenye miamba Mlima K’njaro

Sunday March 23 2014

By Daniel Mjema, Mwananchi

Moshi. Mtalii mmoja raia wa Ujerumani, Jeane Traska (32) amenasa katika miamba ya kilele cha Mawenzi cha Mlima Kilimanjaro baada ya kwenda kinyemela eneo hilo ambalo haliruhusiwi kupandwa na watalii isipokuwa kwa ruhusa maalumu.

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa), Erastus Lufungilo, alilithibitishia gazeti hili jana kuhusu kunasa kwa mtalii huyo pamoja na mwongoza watalii (Guide) aliyejulikana kwa jina la Athman Juma kutoka Kampuni ya Nordic Tours.

“Ni kweli kuna tukio hilo na wote wawili wamenasa huko tangu asubuhi na tunafanya kila jitihada kuokoa maisha yao, lakini kimsingi walikwenda huko kinyemela kwa sababu wao walitakiwa kwenda Kibo lakini wao wakaenda Mawenzi, alisema.

Meneja Uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa Nchini (Tanapa), Paschal Shelutete, aliliambia gazeti hili jana kuwa mtalii huyo pamoja na mwongozaji huyo wa watalii wamenasa katika miamba ya kilele hicho baada ya kamba waliyokuwa wakiitumia kunasa kwenye miamba.

Shelutete alisema mtalii huyo alianza kupanda mlima huo Machi 18 mwaka huu kwa kutumia njia ya Rongai, safari ambayo ingewachukua siku tano, lakini kwa sababu ambazo hazijulikani alibadili njia na kuelekea kilele cha Mawenzi badala ya Kibo.

“Tanapa kwa kushirikiana na kampuni yaNordic Tours tunaendelea na jitihada za kuwaokoa kwa kutumia askari wetu wazoefu pamoja na helkopta itakayosaidia zoezi la uokoaji kwa kutegemea hali ya hewa itakavyotulia. Sasa hivi kuna mawingu mazito”alisema.

Kwa mujibu wa Shelutete, ili mtalii aweze kuruhusiwa kupanda kilele hicho cha Mawenzi ambazo ni miamba, hutakiwa kujaza fomu maalumu ili aweze kubeba dhamana yako mwenyewe endapo utapatwa na matatizo katika kupanda kilele hicho.

 

Advertisement