Mtanzania aliyeshiriki kuunda Dreamliner kutunukiwa tuzo Marekani

Muktasari:

  • Taasisi ya Beya Stem ya Marekani imetoa orodha ya wataalamu wa sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati watakaopewa tuzo mwaka huu akiwemo Mtanzania George Jonas aliyeshiriki kuunda ndege ya Boeing 787-8 Dreamliner iliyonunuliwa na Serikali mwaka jana.

Dar es Salaam. Mtanzania aliyeshiriki katika uundwaji wa ndege Boeing 787-8 Dreamliner iliyonunuliwa na Serikali ya Tanzania Julai 2018, George Jonas ni miongoni mwa wanasayansi waliofuzu kupewa tuzo za mwaka huu katika mkutano wa Beya Stem unaohusisha wataalamu wa sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati.

Utoaji wa tuzo hizo unatarajiwa kufanyika Washington, Marekani Februari 7, 2019 ukiwa ni mwendelezo wa mikutano inayofanywa na Beya Stem kila mwaka.

Jonas amechaguliwa kuchukua tuzo katika kundi la Walt W. Braithwaite Legacy Award akiwa ni mhandisi wa usalama katika ndege za aina ya 777X kutoka kampuni ya Boeing.

Jina la Jonas ambaye ni mwenyeji wa mkoani Mbeya lilianza kuvuma mara baada ya ndege ya Boeing 787-8 ilipotua nchini Julai 8, 2018 akiwa ni miongoni mwa wataalamu waliohusika katika utengenezaji wa ndege hiyo yenye viti 262.