Mteja Standard Chartered kupata huduma 70 bila kukanyaga benki

Muktasari:

  • Benki ya Standard Chartered imezindua program ya simu ambayo inauzwezo wa kutoa huduma 70 zinazotolewa na benki hiyo kwa bei pungufu kwa asilimia 50 ikilinganisha na bei katika tawi.

Dar es Salaam. Benki ya Standard Chartered imezindua mfumo mpya wa teknolojia katika huduma zake ambapo sasa wateja wake wataweza kupata huduma 70 zinazotolewa na benki hiyo bila kufika katika tawi.

Katika uzinduzi wa mfumo huo leo Februari 21, Mkurugenzi Mtendaji wa wa benki hiyo, Sanjay Rughani amesema mfumo huo unaotumia simu za kisasa (Smart phone) unatarajia kuwapatia wateja wapya hadi 40,000 mpaka Desemba mwaka huu.

“Tanzania imekuwa nchi ya tatu kuzindua mfumo huu miongoni mwa Nchi 70 ambazo Standard Chartered tunatoa huduma, mfumo huu unarahisiha huduma kwa kuwa na gharama ndogo za huduma lakini pia kwa kuwa matumizi ya simu ni makubwa utasaidia kujumuisha Watanzania wengi katika huduma za kifedha,” amesema Sanjay.

Kwa upande wake mkuu wa benki hiyo ukanda wa Afrika na Mashariki ya kati Jaydeep Gupta ambaye amehudhuria uzinduzi huo amesema mtumiaji wa programu hiyo ataweza kufungua akaunti bure, kukopa, na kufanya miamala mingine kwa gharama nafuu.

“Kwa kipindi cha miaka mitatu benki imetumia Dola 1.5 bilioni 1.5 katika uboreshaji wa teknolojia mbalimbali, leo tumezindua mfumo huu hapa kesho ni Ghana na mwezi ujao tutazindua Kenya, tutaendelea kufanya hivyo katika nchi nyingine,” amesema Gupta.

Katika hafla hiyo msanii wa Bongo Fleva, Vanessa Mdee ametambulishwa kuwa ndiye balozi wa programu hiyo hapa nchini.