VIDEO: Mtifuano siku 55 Bunge la Bajeti

Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa juzi aliahirisha mkutano wa 15 wa Bunge la Bajeti ulioibua hoja za vuta nikuvute kwa siku 55 katika mjadala wa bajeti 21 za wizara na bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2019/2020.

Katika Bunge hilo lililoanza Aprili 2, yapo mambo mengi yaliyoibuka ya kisheria, kiuchumi na kijamii na baadhi kutolewa ufafanuzi wa Serikali baada ya kutakiwa kufanya hivyo ama na Spika Job Ndugai, naibu wake, Dk Tulia Ackson au wenyeviti wa Bunge; Andrew Chenge, Mussa Zungu na Najma Giga.

Baada ya wizara kuwasilisha bajeti zake, kujadiliwa na kupitishwa, Juni 13 Serikali iliwasilishwa bajeti yake ya Sh33.1 trilioni na kufuatiwa na mjadala wa siku saba uliohitimishwa kwa wabunge kupiga kura kuipitisha na baadaye kuwasilishwa kwa muswada wa sheria ya fedha ambao ulipitishwa juzi.

Bunge kutofanya kazi na CAG

Katika Bunge hilo ilishuhudiwa chombo hicho cha kutunga sheria kikipitisha azimio la kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kutokana na kauli aliyoitoa wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kuwa Bunge ni dhaifu. Kabla ya uamuzi huo, Profesa Assad alihojiwa na kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ambayo ilipendekeza Bunge lisifanye naye kazi na hoja hiyo ikapita.

Mdee na Lema kikaangoni

Kauli ya Mdee na mwenzake Lema kukubaliana na kauli ya Profesa Assad kuwa Bunge ni dhaifu iliwapeleka kuhojiwa na Kamati ya Haki, Maadii na Madaraka ya Bunge iliyopendekeza wasimamishwe kuhudhuria mikutano ya Bunge. Mdee alizuiwa kuhudhuria mikutano miwili na Lema mitatu.

Nyongeza mishahara

Wabunge wengi walihoji kuhusu nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma akiwemo mbunge wa viti maalumu (Chadema), Ruth Mollel.

Ruth, katibu mkuu mstaafu wa Utumishi, alisema tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani haijawahi kuongeza mishahara ya watumishi.

Wakijibu hoja hiyo mawaziri watatu; George Mkuchika (Utumishi na Utawala Bora), Jenister Mhagama (Ofisi ya Waziri Mkuu) na naibu waziri wa Elimu, William Ole Nasha walisema Serikali itatekeleza suala hilo wakati ukifika huku Mkuchika akienda mbali zaidi na kutolea mfano miradi mikubwa inayotekelezwa sasa na Serikali.

Ma-DC na RC washukiwa

Kufuatia vilio vya wabunge tangu kuanza kwa Bunge hilo kuhusu wakuu wa mikoa na wilaya kuwaweka watu ndani, Waziri Mkuchika alisema watakaowaweka watu ndani kinyume cha sheria, watashtakiwa wao binafsi, hawatatetewa na mwanasheria mkuu wa Serikali na akawataka wazingatie sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997.

IMF na Serikali

Suala la Shirika la Fedha Duniani (IMF) kueleza kuwa limezuiwa kuchapisha taarifa ya tathmini ya uchumi wa Tanzania liliibuliwa na baadhi ya wabunge hasa wa upinzani na kupingwa na Serikali.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema Serikali haijazuia kuchapishwa kwa ripoti hiyo bali inaendelea na mazungumzo na IMF.

Ugonjwa wa dengue

Madai kuwa ugonjwa wa dengue ni hatari huku vipimo vyake vikitajwa kuwa bei ghali viliifanya Serikali kutoa tamko bungeni.

Juni 21, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alisema watu wanne ndio walioripotiwa kufariki dunia kwa ugonjwa huo, huku akitangaza kuwa Serikali itatoa vipimo bure kwenye vituo vya afya vya umma.

Sakata la Masele na Ndugai

Spika Ndugai alimtaka Masele kurejea kutoka Afrika Kusini katika vikao vya Bunge la Afrika (PAP) akidaiwa kuzungumza mambo yanayogonganisha mihimili ya dola.

Mbunge huyo alihojiwa na kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iliyopendekeza azuiwe kuhudhuria mikutano mitatu ya Bunge, lakini Ndugai akamsamehe.

Hotuba za upinzani kuhaririwa

Kambi rasmi ya upinzani bungeni ilizuiwa kusoma baadhi ya hotuba zao kama walivyoziandika na badala yake kutakiwa kuzisoma zilizohaririwa na Bunge kwa maelezo kuwa zilikuwa na maneno yasiyo ya kibunge.

Hata hivyo, Ndugai baadaye aliruhusu wapinzani kusoma hotuba walizoziandaa huku akiwatahadharisha kutoweka maneno yanayoweza kusababisha migongano na mihimili mingine. Maoni ya upinzani kuhusu Wizara ya Mambo ya Ndani; Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na na Wizara ya Fedha yaliondolewa.

Miradi Zanzibar kukwama

Wabunge walihoji kukwama kwa miradi mitatu mikubwa Zanzibar ya ujenzi wa barabara ya Wete-Chakechake, uwanja wa ndege wa Abeid Aman Karume (Terminal II) na ujenzi wa bandari ya Mpigaduli.

Katika majibu yake Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema miradi ya ujenzi wa barabara na uwanja umekwama kwa kuwa kifungu cha mkataba kinaitaka Serikali kuweka mali zake kama dhamana ya mkopo ambazo ni mali za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Benki Kuu (BoT), mali kale, mali za kihistoria, mali za ubalozi na mali nyingine zilizoanishwa katika sheria za Tanzania jambo ambalo hawezi kulikubali.

Zanzibar kukopa nje

Suala la Zanzibar kutoweza kukopa nje lilitikisa Bunge hilo huku mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea akihoji lini Serikali itapeleka bungeni marekebisho ya Katiba na sheria ili kuiruhusu Zanzibar kukopa nje kuendesha miradi yake mikubwa.

Hata hivyo, naibu waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji alisema suala hilo lipo kwenye majadiliano katika ngazi ya wataalamu na unaandaliwa waraka kwenda katika baraza la mawaziri kupatiwa ufumbuzi.

Waziri wa zamani wa Fedha, Dk Saada Mkuya alihoji sababu za Bunge kuridhia sheria zinazokinzana na Katiba na kuibua kero mpya ya muungano inayotoa masharti mapya ya Zanzibar kukopa.

Kauli ya Jaguar yatikisa Bunge

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alitoa kauli ya Serikali kuhusu mbunge wa Starehe nchini Kenya, Charles Njagua Kanyi ‘Jaguar’ aliyewapa saa 24 Watanzania waishio Kenya kurejea makwao.

Majaliwa alitoa kauli hiyo baada ya wabunge kuchachamaa wakitaka kauli ya Serikali na kutakiwa na Ndugai kutoa maelezo.

Hotuba kuchanwa

Dk Tulia aliwatoa ndani ya ukumbi, wabunge watatu wa Chadema walioibua zogo bungeni kuhusu uamuzi uliochukuliwa dhidi ya mbunge wa Kasulu Vijijini (CCM), Augustine Vuma aliyechana kitabu cha hotuba mbadala ya bajeti ya kambi rasmi ya upinzani bungeni mwaka 2019/2020.

Wabunge hao ni Esther Matiko (Tarime Mjini), John Heche (Tarime Vijijini) na Dk Emmaculate Sware (Viti Maalumu), waliopinga uamuzi wa Dk Tulia kumtaka Vuma kuomba radhi kwa alichokuwa akizungumza wakati akichana kitabu hicho na si kitendo chake cha kuchana kitabu.

Katazo mifuko ya plastiki

Pia katika mkutano huo, Majaliwa alitangaza kuanzia Juni Mosi, itakuwa ni marufuku kutengeneza, kuuza, kuingiza na kutumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa za aina yoyote jambo ambalo utekelezaji wake umeanza.

Sakata la Taifa Stars

Kauli ya kiongozi mmoja kijana wa Dar es Salaam kwamba wabunge wameidhihaki Taifa Stars inayoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) liliibua zogo bungeni na kumlazimu Ndugai kusema kuna kiongozi kijana wa Serikali alimdanganya Rais wakati hakuna sehemu yoyote ambayo wawakilishi hao wa wananchi waliwadhihaki wachezaji.

Ujenzi Bandari Bagamoyo

Suala la ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo mkoani Pwani liliibuka katika Bunge hilo baada ya Ndugai na wabunge kuitaka Serikali kutoa ufafanuzi wa kwa nini mradi huo hautekelezwi licha ya kuwa na tija kwa Taifa endapo ungekamilika.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema majadiliano kati ya wawekezaji wanaotaka kujenga yanaendelea yatakapofika mwisho taarifa yake itatolewa.

Wabunge kuhongwa

Wabunge wa Chadema, Cecil Mwambe (Ndanda) na Salome Makamba (Viti Maalumu) waliomba Bunge kuzifanyia kazi tuhuma kuwa wabunge wamepewa rushwa na taasisi 30 zisizo za kiserikali (NGO) zilizokutana nao jijini Dodoma kueleza ubaya wa muswada namba tatu wa marekebisho ya sheria mbalimbali wa mwaka 2019 uliowasilishwa bungeni na Serikali.

Katika majibu yake, Dk Tulia aliwataka wabunge hao waliotajwa kupewa rushwa kuvishtaki vyombo husika mahakamani, kwani ofisi ya Bunge haina taarifa ya kufanyika kwa mkutano huo.