Mtoto wa miaka sita awa polisi Marekani

Muktasari:

  • Familia ya Abigail Arias ilihudhuria hafla ya kuapishwa kwa mtoto wao huyo kuwa polisi

Texas, Marekani. Askari Polisi wa Marekani ametokwa machozi wakati akimwapisha kwa heshima mtoto Abigail Arias (6) kuwa polisi.

Mtoto huyo anayesumbuliwa na saratani ya kibofu kwa miaka miwili sasa alihudhuria hafla hiyo ya kuapishwa akiwa na familia yake, huku akisema anaipenda kazi hiyo na ataifanya kwa weledi.

Polisi wa Texas, walituma taarifa za kumwapisha mtoto huyo katika hafla iliyofanyika mjini hapo kuwa polisi wa mji wa Freeport wenye watu 12,000 uliopo maili 50 kutoka Kusini mwa Houston.

Polisi amwaga machozi

Ofisa wa polisi aliyekuwa akimwapisha mtoto huyo alishindwa kujizuia na kuanza kulia kwa kwikwi huku akimkumbatia baada ya kumaliza kumwapisha.

“Nitapambana na wahalifu’’ hayo ni maneno ya mtoto huyo aliyotoa baada ya kuapishwa huku akishangaza wengi waliokuwa wamehudhuria hafla hiyo

Wakati akiapishwa mtoto huyo alikuwa amevalia vazi la polisi ambalo lilimpendeza na kumfanya kuwa na faraja wakati wote wa hafla hiyo iliyokuwa imehudhuriwa na familia yake pia na maofisa kadhaa wa polisi.

Mama mzazi wa mtoto huyo aliyefahamika kwa jina la Ilene Arias, aliliambia Shirika la Habari la CNN kwamba huu ni muda wa kufurahia maisha ya mtoto huyo kwani watalia wiki chache zijazo.

Mama huyo alitoa kauli hiyo huku akiwa anabubujikwa na machozi mbele ya waandishi wa habari, akimaanisha kwamba mtoto wake huyo hawezi kuendelea kuishi kwa muda mrefu.

Kilio cha mama huyo kinakwenda sawa na polisi aliyekuwa akimwapisha ambaye alishindwa kujizuia na kuanza kulia Kamanda huyo wa Freeport, Raymond Garivey, alisema mtoto huyo anaishi kwa nguvu za Mungu tu.

“Tunatakiwa kumuombea mtoto huyu kwa sababu inafahamika anaumwa kitu gani hapa anaishi kwa miujiza tu, hivyo tumuombee,’’ alisema.

‘’Nataka kuhakikisha ndoto zake zinatimia na kuwa za kweli hivyo leo tumemwapisha kuwa askari kamili wa Marekani kwa sababu ilikuwa ni ndoto yake ya muda mrefu,’’ alisema.

Baada ya kuapishwa kuwa askari Arias alikabidhiwa ofisi na bunduki kama walivyo askari wengine huku akionyesha tabasamu.