Mtoto wa siku moja akutwa amekufa katika sinki la choo

Kamanda wa polisi mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley

Muktasari:

Mtoto anayedhaniwa wa siku moja atupwa kwenye choo cha Shule ya Sekondari Kazima na kuokotwa akiwa amefariki.

Tabora. Mtoto anayekadiriwa kuwa wa siku moja amekutwa kwenye choo cha Shule ya Sekondari Kazima mkoani Tabora akiwa ametanguliza kichwa na miguu kuwa nyuma.

Mtoto huyo ambaye alikuwa amekufa, kichwa kimeonekana kama kilikuwa kimelazimishwa kwa nguvu kuingizwa katika tundu la choo maalum cha kumwagia maji, wengi huviita vyoo vya kuflashi.

Mkuu wa Sekondari ya Kazima, Mrisho Kivuruge akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Aprili 19, 2019 amesema jana usiku saa nne kasorobo, walipata taarifa za kuonekana mtoto kwenye choo cha shule.

Amesema choo alichokutwa mtoto huyo ni vya madarasa ambavyo ni vya wazi na hutumika pia na wapita njia.

Ameeleza waliamua kuwabana wanafunzi kwa kuwataka wawe kwenye mabweni yao na kuitwa majina.

"Tuliamua kuwafanyia vipimo na nashukuru hakuna aliyeonekana kuhusika," amesema.

Ameongeza kuwa wana utaratibu wa kuwapima wanafunzi na ili kugundua mapema kama mwanafunzi ana ujauzito.

Mwalimu Mrisho amesema aliyefanya unyama huo ili asijulikane atakuwa ni mtu wa uraiani na si mwanafunzi.

Akizungumzia tukio hilo, kamanda wa polisi mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley amesema limetokea usiku saa tatu na hakuna anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo.

Kamanda Nley amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa lengo la kumbaini mhusika wa tukio kwanza kwa kumtambua aliyekuwa mjamzito au aliyejifungua.

Amesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na kuomba ushirikiano wa wananchi.

Mmoja wa majirani wa shule hiyo aliyeomba hifadhi ya jina lake amesema mfanyaji wa tukio hilo atakuwa ni mtu kutoka nje ya eneo hilo.

"Katika maeneo haya kimsingi tunafahamiana, hakuna aliyekuwa mjamzito, mhusika atakuwa anatoka nje ya hapa," amesema.

Mhusika inaonekana hakuwa mzoefu wa aina hizo za vyoo kwani inaonekana  alilazimisha kutaka kukasukuma katoto kwa kutumia maji utadhani ni kinyesi na hivyo kukasukuma kwa nguvu na kushindwa.

Ili kumtoa mtoto huyo mchanga ilibidi watu wabomoe choo hicho na kukatoa na sasa choo hicho kimefungwa hakitumiki.