Mufti awataka wanaofuturisha kufuata maadili ya Kiislamu, waache kupiga muziki

Muktasari:

Wakati mfungo wa Ramadhan ukiwa katika siku ya 20, Mufti wa Tanzania ataka wanaofuturisha kufuata maadili ya Uislamu

Dar es Salaam. Mufti wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zubeir amewataka wadau wanaofuturisha katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye mahoteli kufuata na kulinda maadili ya Uislamu kwenye shughuli hiyo.

Muft Zubeir ametoa kauli hiyo, leo Jumapili Mei 26, 2019 wakati  wa fainali ya tuzo ya kimataifa ya kuhifadhi Qur'an yaliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam.

Fainali hizo zimeandaliwa na Jumuiya ya Kuhifadhi Qur'an Tanzania, Zimehudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Makamu wa Rais mstaafu, Dk Mohammed Gharib Bilal na Waziri wa Ulinzi na Jeshi LA Kujenga Taifa (JKT), Dk Hussein Mwinyi.

Mufti Zubeir amesema, “siyo mnafuturisha watu huku mnapiga muziki. Wale wanaohudumia hasa kina mama wavae mavazi yenye utamaduni wa Kiislam," amesema Zubeir.

Akizungumzia mashindano hayo, Zubeir amewashukuru waandaaji kwa kujipanga vyema katika mchakato huo huku akisema yamejikita kuwafundisha watoto katika maadili mema.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kuhifadhi Qur'an Tanzania, Athuman Kaporo amesema mashindano hayo ni ya 27 tangu kuanzishwa kwake na ameishukuru Serikali kwa ushirikiano wao kwenye mchakato huo.