Muhimbili yaokoa Sh2.24 bilioni upandikizaji figo

Muktasari:

  • Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeokoa Sh2.24 bilioni kutokana na kutokana na kutoa huduma ya kupandikiza figo. Upandikizaji wa figo ni miongoni mwa magonjwa yanayotibiwa kwa fedha nyingi hivyo huduma hiyo kutolewa nchini ni unafuu mkubwa. Matibabu mengine ghali zaidi ni upandikizaji wa vifaa vya usikivu kwa watoto.

Dodoma. Kutokana na wagonjwa 29 waliopandikizwa figo kati ya Julai mwaka jana na Machi mwaka huu, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeokoa Sh2.24 bilioni.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema gharama ya huduma hiyo ni kati ya Sh20 milioni hadi Sh30 milioni nchini ikilinganishwa na kati ya Sh100 hadi Sh120 milioni zinazotozwa katika hospitali za nje ya nchi kwa mgonjwa mmoja.

Kutokana na wagonjwa waliohudumiwa katika kipindi hicho, Ummy amesema imefanya idadi ya waliopandikizwa figo kufika 38 tangu huduma hiyo ilipoanza kutolewa Novemba 2017.

Hospitali hiyo pia ilipandikiza vifaa vya usikivu kwa watoto 11 waliolipia kati ya Sh35 milioni na Sh40 milioni. Awali, kabla ya Juni 2017, huduma hiyo ilikuwa inapatikana nje ya nchi kwa gharama ya kati ya Sh80 milioni na Sh100 milioni.

Tangu ilipoanza kutolewa, Ummy amesema jumla ya watoto 21 wamehudumiwa na kuokoa zaidi ya Sh840 bilioni.

Kutokana na kuimarika kwa huduma za kibingwa nchini, idadi ya wagonjwa wanaopewa rufaa kwenda kutibiwa nje ya nchi ilikuwa 62 ikijumuisha saratani (16), moyo (15), mifupa (12), mishipa ya fahamu (6), mishipa ya damu (5), figo mmoja na mengineyo (7).

Atika kipindi hicho, waziri huyo amesema jumla ya wagonjwa 419,931 walihudumiwa Muhimbili kati ya wagonjwa milioni 1.42 waliotibiwa katika hospitali za rufaa za kanda, hospitali maalumu na hospitali ya taifa. Kwa idadi hiyo ya wagonjwa iliyohudumia, Muhimbili ilivuka lengo la 300,000 ililojiwekea.

Alitoa taarifa hiyo jana Mei 7 alipowasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2019/20.