MAWAIDHA YA IJUMAA: Muislamu na malezi ya nafsi yake

Uislamu ni dini ya maumbile kutoka kwa Mwenyezi Mungu na imemwelekeza mwanadamu jinsi ya kuishi duniani, ili baada ya kifo akaishi maisha yenye raha na amani ya milele.

Moja katika mambo ambayo Uislamu umemwelekeza mwanadamu ni jinsi ya kuilea nafsi yake, ambapo imemfundisha usafi wa nafsi, mwili, matendo ya kibinafsi na yale ya kijamii na mazingira yake kwa ujumla.

Haya yote ni maandalizi ya kumwezesha Muislamu kuubeba ujumbe wa mwisho wa Mwenyezi Mungu kwa wanadamu.

Katika hadithi ya Swahaba Handhwallah, Allah amrehemu, Mtume rehma na amani ziwe juu yake aliwaambia baadhi ya Maswahaba zake waliokuwa wanarejea kutoka safari;

“Hakika mnakwenda kwa ndugu zenu basi wekeni vizuri mizigo yenu na vaeni mavazi yenu mazuri mpaka muwe na muonekano wenye mvuto mbele za watu, kwani Mwenyezi Mungu hapendi mambo ovyo ovyo wala mwenye muonekano wa ovyo ovyo” (Imepokewa na Abuu Dawuud).

Hapa Mtume anawafundisha Maswahaba wake utanashati na ustaarabu katika mambo yao ili muonekano wao wa nje uwe wa kuvutia watu. Maana yake ni kwamba watumie fedha kununua mavazi mazuri mazuri na kila chenye kufanya muonekano wao uwe mzuri, kwani ni jambo linalompendeza Mwenyezi Mungu.

Kuitendea haki nafsi

Muislamu wa kweli haipuuzi nafsi yake pamoja na majukumu makubwa anayoyabeba katika kumuabudu na kumtumikia Mwenyezi Mungu na majukumu mengine ya kimaisha.

Kwa hiyo anahakikisha ameweka mizania kati ya kujishughulisha na maisha na ibada na kuihudumia nafsi na akili yake.

Anafanya hivyo ili kukipa kila kimoja haki zake na wala hajikiti katika kimoja na kusahau kingine. Hajikiti katika kumuabudu tu Mwenyezi Mungu na akaupuuza mwili wake au nafsi yake.

Mwenyezi Mungu anasema: “ Na mbingu ameziinua na akaweka mizani. Basi msichupe mipaka katika mizani.” (Qur’an 55:7-8).

Uislamu unamfundisha mwanadamu kuweka mizani katika kila jambo. Mtume rehma na amani ziwe juu yake ambaye alikuwa na tabia ya kukiweka kila kitu mahali pake, alitupa mwongozo alipomuuliza Swahaba Abdallah ibn Amr ibn al ‘As:

“Je sikupewa habari kwamba wewe unafunga swaumu kila siku na unasimama kila usiku kwa ibada? Akajibu ‘ndiyo ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu.

Mtume akamwambia basi usifanye hivyo, funga na siku nyingine fungua na simama usiku na siku nyingine lala kwani hakika mwili wako una haki juu yako na macho yako yana haki juu yako na mke wako ana haki juu yako na mgeni wako pia ana haki juu yako” (Bukhari na Muslim).

Tazama uzuri wa Uislamu; hapa Mtume anatufundisha kwamba si ucha-Mungu Muislamu kujitaabisha tu kwa matendo ya ibada na akasahau haki au mahitaji ya mwili wake, haki za mke wake na hata wageni wake.

Jinsi ya kuweka mizania katika maisha

Swali linalokuja ni vipi Muislamu ataweka mizania katika maisha yake ili kuyapa umuhimu mkubwa mambo ya kimwili kusizidi yale ya kiroho au kinyume chake?

Haki za mwili; Katika kuupa mwili haki ni kuhakikisha kwamba unapata lishe inayotakiwa, ikiwa ni pamoja na kula na kunywa maji vyote kwa ubora na kiwango kinachotakiwa.

Afya ya mwili ni jambo muhimu na la kwanza kuangaliwa kwa sababu mtu asiye na afya njema hawezi kutekeleza majukumu yake ipasavyo iwe ni yale ya kiibada, ya binafsi au ya kijamii.

Ili kuwa na afya njema, muumini hula pale kula kunapohitajika tu na hali ovyo ovyo. Kwa hiyo anaizuia nafsi yake na tabia ya kula kula ovyo hata kama ni vya halali.

Mwenyezi Mungu anasema: “Na kuleni na kunyweni na wala msifanye ubadhirifu hakika yeye hapendi wafanyao ubadhirifu” (Qur’an 7:31).

Na Mtume anasema: “Mwanadamu hakupata kujaza chombo chenye madhara kuliko kujaza tumbo lake. Na ikiwa hapana budi kula sana basi theluthi iwe kwa chakula chake, theluthi kwa maji yake na theluthi kwa ajili ya pumzi zake” (Ahmad, Tirmidhy).

Khalifa Umar naye anasema: “Jiepusheni na kujaza tumbo kwa vyakula na vinywaji, kwani ni vyenye kuuharibu mwili na vinasababisha maradhi na kutia uvivu wa swala. Na pendeni kuwa na kiasi katika vyakula na vinywaji, kwani ndiyo sawa kwa mwili na kuwa mbali na ubadhirifu. Hakika Mwenyezi Mungu anamchukia mtu mnene na hakika mtu hatoangamia mpaka matamanio yake ya nafsi yazidi dini yake” (Kitabu Al-Kanzu, Mjalada 8/47)

Lakini tazama tabia tuliyonayo Waislamu wa zama hizi kuhusu kula na kunywa jinsi tunavyofanya ubadhirifu mkubwa utadhani hatuna mwongozo kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Jamii za Kiislamu hasa wale wenye uwezo mkubwa kifedha, ndizo zinazosifika kwa kumwaga majalalani vyakula vilivyobakia majumbani baada ya kula.

Inakadiriwa kwamba mwezi wa Ramadhani katika nchi za Kiislamu ubadhirifu wa vyakula, husababisha upotevu mkubwa wa fedha ambazo zingetumika kwa mambo yenye manufaa.

Kwa mfano, mwaka 2012 manispaa ya mji wa Dubai ilikadiria kwamba kiasi cha tani 1,850 za chakula kilitupwa majalalani kwa siku moja wakati wa mwezi wa Ramadhan.

Mwaka huo huo, nchini Bahrain zaidi ya tani 400 za vyakula zilimwagwa kwa siku. Hata kama kinachomwagwa ni kilo moja kwa siku, bado huo ni ubadhirifu katika vyakula, jambo ambalo limeharamishwa.