Museveni amuandikia Kagame barua kuzungumzia tuhuma za kusaidia waasi

Muktasari:

Amedai kwamba hahusiki na tuhuma za kushirikiana na waasi wanaoipinga Serikali ya Rwanda  kama inavyodaiwa 

Kampala, Uganda. Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amemwandikia barua kiongozi mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame kuhusu madai ya kuhifadhi waasi wa nchi hiyo jirani.

Barua hiyo iliandikwa Machi 10 baada ya kukutana na raia wawili wa Rwanda ambao serikali ya nchi hiyo inadai wanatoka kundi la waasi la Rwanda National Congress (RNC). 

Raia hao ni Charlotte Mukankusi na mfanyabiashara Tribert Rujugiro Ayabatwa, anayemiliki miradi mingi mikubwa nchini Uganda na nchi nyingine.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, japokuwa Museveni alimuandikia Kagame kuhusu mazingira aliyokutana na watu hao, Serikali ya Rwanda imekuwa ikibadili habari hiyo na kudai  Museveni anaiunga mkono RNC.

Shirika la habari la Rwanda la KTpress, lililo karibu na Serikali ya Rwanda, liliripoti hivi karibuni kuwa kuna ushahidi wa Rais Museveni kuliunga mkono kundi hilo la kigaidi ili kuiyumbisha Rwanda.

“Machi 1, 2019, mkuu wa diplomasia wa RNC, Charlotte Mukankusi, alikuwa jijini Kampala, alipokutana na Rais  Yoweri Museveni. Mukankusi alikuwa naibu wa Kayumba Nyamwasa wakati  kiongozi huyo wa RNC alipokuwa balozi wa Rwanda nchini India,” lilisema KTpress.

Hata hivyo, gazeti la New Vision la Uganda limeona nakala ya barua ya Museveni aliyoiandika kwenda kwa  Rais  Kagame, Machi 10, 2019, ikielezea mazingira aliyokutana na Mukankusi.

Katika barua hiyo, Museveni anasema Mukankusi alimtaka asaidie kulipiza  kisasi cha kifo cha mumewe Rutagarama aliyeuawa na Serikali ya Rwanda, lakini alimkatalia akisema asingeingilia masuala ya Rwanda.

Kuhusu Rujugiro, yeye alizungumza naye kuhusu masuala ya biashara zake  nchini Uganda na kumwambia kwamba kama kulikuwa na matatizo mengine alimshauri ayapeleke kwenye mahakama za Uganda.

Awali Rais Kagame alielezea kuwa chimbuko la mgogoro baina ya nchi yake na nchi ya Uganda ni la tangu miaka 20 iliyopita nchi ya Uganda ikitaka kuangusha utawala wake.

Akihutubia mkutano wa kitaifa Rais Kagame alisema  mgogoro huo ulishika kasi miaka ya hivi karibuni kutokana na Serikali ya Uganda kuunga mkono kundi hilo la RNC.