Musukuma aipa angalizo Morogoro

Muktasari:

Mradi wa ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi cha Msamvu na soko kuu ni miradi ya kimkakati ambayo mbali ya kusaidia kuongeza mapato ya Halmashauri lakini pia imelenga kukuza uchumi wa nchi.

Morogoro. Mbunge wa Geita (CCM), Joseph Kasheku maarufu Musukuma ameishauri Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuongeza vyanzo vya mapato katika kituo cha mabasi ya mikoani na nje ya nchi cha Msamvu mkoani humo badala ya kutegemea chanzo kikubwa cha ushuru wa mabasi yanayoingia katika kituo hicho.

Msukuma ametoa ushauri huo leo Ijumaa Aprili 19,2019 baada ya kamati ya fedha ya halmashauri ya Geita kufanya ziara ya kujifunza katika kituo hicho, ambapo amesema pamoja na kujengwa kwa kituo hicho cha kisasa kama halmashauri ya manispaa ya Morogoro haitabuni vyanzo vya kutosha vya mapato ipo siku itashindwa kuendesha kituo hicho.

Amesema wamiliki wa mabasi akiwamo yeye mwenyewe wapo kwenye mchakato wa kubadilisha sheria ya ushuru wa mabasi unaotozwa kila kituo kwa kuwa umekuwa kero na pia unasababisha hasara ambapo katika mchakato huo wameomba walipe ushuru kwenye kituo kinachoanzia safari na kumalizia safari.

“Sheria hii ikifanyiwa mabadiliko tutakuwa tunalipa ushuru kituo cha kwanza cha safari na cha mwisho na ndio kituo hiki cha msamvu kitakapokosa mapato na itafika mahali kigeuzwe kuwa uwanja wa mpira, wahusika nawapa angalizo mapema,” amesema Musukuma.

Katika ziara hiyo ya mafunzo kamati ikiongozwa na mkuu wa wilaya ya Geita, Josephati Maganga imetembelea pia mradi wa ujenzi wa soko kuu la kisasa ambapo ujenzi unaendelea hata hivyo wameipongeza halmashauri ya manispaa ya Morogoro kwa kujenga soko hilo ambalo litakuwa chanzo kikubwa cha mapato.

Maganga amesema kupitia ziara hiyo wameona miradi hiyo mikubwa na ya kisasa hivyo wamejifunza mengi ikiwa ni pamoja na kujenga soko litakaloweza kuhudumia watu wa kipato cha chini, kati na cha juu.

 

Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Morogoro, Pascal Kihanga amesema ujenzi wa soko hilo ulikuwa na changamoto mbalimbali ikiwamo kuwaondoa wafanyabiashara waliokuwa wakifanya biashara kwenye soko la zamani.

Hata hivyo, Kihanga amesema kutokana na viongozi wa halmashauri hiyo kuwa na msimamo, ushirikiano walifanikiwa kuwahamisha wafanyabiashara hao bila vurugu hata hivyo baada ya kukamilika wafanyabiashara hao watapewa kipaumbele kwa kuwapatia vizimba vya kufanyia biashara kwa gharama nafuu itakayopangwa na halmashauri.

Akitoa taarifa za miradi hiyo, Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Michael Waluse amesema mradi wa ujenzi wa kituo cha mabasi umegharimu zaidi ya Sh14 bilioni na ujenzi wa soko utagharimu Sh17.6  bilioni.

Waluse amesema makusanyo ya mapato katika kituo cha mabasi Msamvu kwa siku sio chini ya Sh3 milioni hata hivyo gharama za uendeshaji ikiwamo kulipa maji, umeme, usafi na mishahara ya watumishi wanaosimamia kituo hicho kwa mwezi sio chini ya Sh 25 milioni.