Muswada wa vyama vya siasa waendelea kupingwa

Dar es Salaam. Wadau wa siasa waliokutanishwa na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), wameukosoa na kuupinga muswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa, baadhi wakisema haupaswi kufika bungeni, lakini CCM imeutetea.

Mikakati ya kuukwamisha muswada huo uliosomwa kwa mara ya kwanza bungeni mwishoni mwaka jana ni mwendelezo wakati kesho Mahakama Kuu ikitarajiwa kutoa uamuzi wa pingamizi la Serikali dhidi ya kesi iliyofunguliwa na wanasiasa watatu akiwamo kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe wanaopinga usijadiliwe bungeni.

Wakati Mahakama ikitarajiwa kutoa uamuzi huo, jana katika mjadala wa wazi uliofanyika jijini Dar es Salaam uliohudhuriwa na baadhi ya wabunge akiwemo John Mnyika (Kibamba-Chadema), aliyeishauri TLS kuhakikisha muswada huo hauingii bungeni.

“Kwa muundo wa Bunge ulivyo sasa, tukifikiria kuwaachia wabunge na kuachia process (mchakato) ya kibunge iendelee mpaka mwisho, nadhani mambo mabovu yaliyoelezwa katika muswada yataendelea,” alisema Mnyika ambaye ni naibu katibu mkuu wa chama hicho (Bara).

“Ni vyema wadau wengine mlioshiriki mkutano huu mkashirikisha taasisi nyingine za dini na kiraia ziende kwa wingi mbele ya kamati ya Bunge zihakikishe kwamba huu muswada usiende mbele ya Bunge, uondolewe.”

Hata hivyo, katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole aliutetea akiwataka wapinzani kutowatisha wananchi kuhusu muswada huo.

“Tusianze kutishwa katikati ya mchakato, tusianze kujenga taswira ya kukataza kuvuka mto kabla hatujafika darajani,” alisema Polepole.

“Sasa hivi tunazungumza ndiyo maana tumepewa nyaraka, tuachwe tuzungumze tusitishwe kwa kuweka kauli timilifu. Ondoa kabisa hii, isisogee karibu na ukumbi wa Bunge, ikifika huko itakuwa balaa. Itakuwa balaa umeshafika?”

Akifafanua, Polepole alisema muswada huo unaweka utaratibu utakaoimarisha vyama vya siasa kitaasisi vitakavyowapa haki wananchi ya kushiriki siasa.

Alisema, “Tunapozungumzia leo hapa masuala ya fedha, tusikimbilie fedha, fedha zilimuua Yesu pia. Hata leo, lazima tuhakikishe kwamba fedha kwenye vyama vya siasa zina utaratibu mzuri. Hatuwezi kuchukulia poa masuala ya fedha kwenye utaratibu wa vyama.”

Naye Zitto ambaye ni mbunge wa Kigoma Mjini akizungumzia suala la ukaguzi wa fedha za vyama, alisema wapinzani ndiyo walioshinikiza suala hilo bungeni.

“Mimi nikiwa naibu katibu mkuu wa Chadema na waziri wa fedha kivuli mwaka 2009 ndiye nilipewa jukumu la kuandaa schedule of amendments (utaratibu wa mabadiliko) ya sheria ya vyama vya siasa ambayo ilimpa mamlaka Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kukagua hesabu za vyama na wabunge wa CCM waligoma, mpaka muswada ukaja mara ya pili,” alisema Zitto.

Madaraka msajili

Awali, akiuchambua muswada huo katika mada yake, wakili maarufu nchini, Harold Sungusia, alisema unampa madakaka makubwa msajili wa vyama vya siasa kuliko hata Rais.

“Msajili anaweza kuamua usajiliwe au usisajiliwe, ufutwe au usifutwe, uwe mwanachama au sio, unafaa kuwa mgombea au hufai, aina gani ya elimu ya uraia inayotakiwa na nani atoe, upewe ruzuku au usipewe,” alisema Sungusia.

“Je, akimfuta uanachama Rais? Yaani msajili ana mamlaka kuliko Rais. Ni jambo kubwa la kikatiba.”

Kauli hiyo iliungwa mkono na mwenyekiti wa Chama cha UPDP, Fahmi Dovutwa aliyesema: “Hali itakuwaje siku msajili amekwenda kwao, ameandika tangazo huko kuanzia leo Rais wa Jamhuri ya Muungano si mwanachama, akatuma katika mtandao, akaenda nje ya nchi Rwanda, Burundi, Congo sasa hali itakuwaje? Nchi itakuwaje?”

Baadhi ya wanajopo waliojadili muswada huo akiwemo Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Benson Bagonza alisema hauakisi matakwa ya vyama vya siasa bali ya msajili.

“Muswada una ujasiri mkubwa wa kuingilia haki za wengine. Kuna hatari ya kujenga mazoea ya kuwa na ujasiri wa vyombo vingine kuingilia haki za wengine,” alisema.

Kwa upande wake, Dk Azaveli Lwaitama aligusia mamlaka ya msajili akisema ni mwendelezo wa utamaduni wa watu kupenda madaraka.

Kuhusu haki za wanawake, mhadhiri wa sanaa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Vicencia Shule alisema muswada huo ulipaswa kuangalia suala hilo kwani vyama vimetawaliwa na mfumo dume.

Naye Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda aliwataka wabunge kutofanya makosa akisisitiza muswada huo usipitishwe.