Muuguzi Mount Meru asimamishwa kazi mwaka mmoja

Muktasari:

  • Baraza la Uuguzi na Ukunga limemsimamisha kazi muuguzi katika hospitali ya Rufaa Mount Meru Arusha baada ya kumtia hatiani na makosa mawili likiwemo la kulewa na kuwasumbua wagonjwa na ndugu zao

Dar es Salaam. Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, limemsimamisha kazi ya kutoa huduma za uuguzi na ukunga kwa mwaka mmoja, Martin Chama wa Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru Arusha.

Uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha baraza hilo cha 196 baada ya kumtia hatiani kwa makosa mawili kati ya manne yaliyowasilishwa katika baraza hilo Septemba mwaka jana na aameanza kuitumikia adhabu hiyo tangu Februari 7, 2019.

Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga, Agnes Mtawa ameyataja makosa hayo kuwa ni kufika kazini akiwa amelewa na kutaka kuhatarisha usalama wa wagonjwa na ndugu zao kwa kushindwa  kutoa huduma kwa umakini na weledi.

“Awali ofisi ya msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga ilipokea tuhuma kutoka Hospitali ya Mount Meru Arusha kupitia kwa muuguzi mkuu wa mkoa ambaye pia ni msimamizi wa maadili wa mkoa wa Arusha kwa mujibu wa sheria N0 1 ya mwaka 2010,” amesema.

Amefafanua kuwa kwa mujibu wa taarifa za awali Septemba 29 Chama alikuwa zamu ya usiku majira ya saa tatu usiku alifika kazini akiwa amelewa.

Akiwa amelewa Chama anadaiwa alianza kuwasumbua ndugu waliokuwa wakiwaangalia wagonjwa wao kutaka kuendelea kutoa huduma kwa wagonjwa ili hali akiwa amelewa sana hali ambayo ingeweza kuhatarisha maisha ya wagonjwa kwa kuwa hakuwa na umakini.

Mtawa amesema tuhuma hizo ziliwasilishwa na walalamikaji wawili waliokuwa wakiuguza wagonjwa wao.

“Kufuatia suala hilo ofisi ya msajili ilituma ofisa kutoka Baraza la Uuguzi na Ukunga ambaye aliungana na timu ya mkoani Arusha ikiongozwa na muuguzi mkuu mkoa wa Arusha.Timu hii ilifanya uchunguzi wa awali na kubaini mapungufu yaliyofanywa na muuguzi huyu ambayo ni kinyume na maadili ya kazi hii,” amesema Mtawa.

Amesema taarifa hiyo ilipelekwa katika kikao cha dharura cha bodi cha 195 ambacho pamoja na mambo mengine ilijadili taarifa hii na kuamua shauri hilo lisikilizwe katika kikao cha bodi cha 196 ambacho kitahusisha mtuhumiwa na mashahidi ambao ni walalamikaji na watumishi waliokuwepo siku ya tukio.

“Tumesikiliza shauri hilo Februari 7 ushahidi uliotolewa umemtia hatiani Martini kwa kulewa na kushindwa kutoa huduma kwa wagonjwa kwa weledi na kutaka kuhatarisha maisha ya wagonjwa na ndugu zao, baraza liliadhimia kwa kauli moja kumsimamisha kutoa huduma hizi kwa muda wa mwaka mmoja.”

Kuhusu baraza

Baraza la Uuguzi na Ukunga ni mamlaka iliyoanzishwa kisheria na kufanya kazi chini ya Sheria inayoitwa (The Nursing and Midwifery Act, of 2010). Baraza lilianzishwa ili kulinda umma kutokana na huduma zinazotolewa na wauguzi na wakunga nchini na linafanya kazi kwa kusimamia ubora katika mafunzo na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinazingatia viwango vilivyowekwa.