Mvua kubwa Kilimanjaro, Arusha wananchi watahadharishwa

Thursday February 14 2019

 

By Pamela Chilongola, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA) imesema baadhi ya maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki ikiwemo mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kuna uwezekano wa kunyesha mvua kubwa zinazoweza kusababisha mafuriko.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Februari 14, 2019 na  mkurugenzi mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi alipokuwa akitoa utabiri wa msimu wa mvua za masika kipindi cha Machi hadi Mei, 2019.

Amesema athari zinazoweza kujitokeza kutokana na kunyesha kwa mvua hizo ni mafuriko, upotevu wa mali, uharibifu wa makazi na watu kupoteza maisha.

Amesema mvua katika maeneo hayo zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya Februari, 2019 na kwamba zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani hadi wastani katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha huku Manyara wakitarajia kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

“Menejimenti ya maafa, watoa huduma za dharura pamoja na wadau wengine wanashauriwa kuchukua hatua za kuweka mipango stahiki kuhakikisha utayari wa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza,” amesema Dk Kijazi.

Amesema mvua za wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi nchini yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.

Hata hivyo, amesema  baadhi ya maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

Amesema Mikoa ya Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga katika wiki ya pili ya Machi, 2019 mvua itanyesha ikitarajiwa kuwa ya wastani hadi juu ya wastani.

Kijazi amesema maeneo machache ya Mkoa wa Kagera na Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma yanatarajiwa kuwa na upungufu wa mvua.

Amesema katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro na visiwa vya Unguja na Pemba katika wiki ya kwanza Machi, mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani.

Amebainisha kuwa maeneo machache ya Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro yanatarajiwa kuwa na upungufu wa mvua.

 


Advertisement