Mvua zafunga barabara kubwa Dar

Muktasari:

Mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es salaam zimesababisha kufungwa barabara ya Morogoro kati ya Magomeni na kituo cha Fire huku barabara nyingine zikifurika magari na kusababisha adha ya usafiri wa abiria na watumiaji magari binafsi

Dar es salaam. Mvua zinazoendelea katika Jiji la Dar es salaam zimesimamisha na kuathiri baadhi ya shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii.

Mvua hizo zimesababisha kufungwa kwa barabara ya Morogoro kati ya Magomeni na kituo cha Fire huku barabara nyingine zikifurika magari na kuwafanya wananchi kuchelewa kufika katika shughuli zao za kiuchumi na nyinginezo.

Njia nyingine iliyofungwa na kuzuia magari kupita ni maeneo ya Kigogo-Jangwani kupitia makao makuu ya klabu ya Yanga.

Mwananchi Digital imepita barabara ya Kawawa, Bonde la Mkwajuni wakati wa asubuhi na kushuhudia maji yakiwa yamejaa na kusababisha magari kupita kwa tabu.

Katika barabara hiyo, foleni ya magari ilionekana kuanzia Kinondoni Mkwajuni, Magomeni Mikumi, Msimbazi –Kigogo ambako magari yalikuwa mengi huku yakienda taratibu kuanzia saa 4:00 asubuhi.

Hatua hiyo imesababisha adha ya usafiri wa abiria na watumiaji wa magari binafsi.

Baada ya kufungwa kwa kipande cha Magomeni Mapipa hadi Fire, madereva wa bodaboda wametengeneza kituo cha muda ndani ya eneo la Kituo cha Mwendokasi wakisubiri abiria. Hali hiyo imeonekana kuanzia saa 5:00 asubuhi.

Mwandishi wa gazeti hili ameshuhudia abiria wakiwa eneo hilo, baadhi wakitumia bodaboda kuzunguka ili  kuingia Posta na wengine wakisubiria daladala zilizoanza kufanya safari fupi ya kuzunguka kutoka eneo hilo kuingia Kariakoo, Mnazi mmoja au Posta.

Katika barabara ya Nyerere, eneo la kuanzia kituo cha Kamata, Maji yamejaa barabarani, huku magari yakipita kwa tabu. Foleni pia ni kubwa kama ilivyoonekana katika Barabara ya Samora, kutoka Posta mpya hadi makutano ya Barabara ya Uhuru na Bibi Titi. Hali hiyo imeonekana hadi saa 7:00 mchana.

Baadhi ya watu waliozungumzia adha hiyo wameiomba Serikali kuimarisha zaidi miundombinu ya jiji pamoja na kupanua njia za michepuko ili kuepuka athari zinazojitokeza kila msimu wa mvua.

Mohamed Khatibu, mkazi wa Kariakoo ameitupia lawama Serikali kwa kuwaondoa wakazi mabondeni huku yenyewe ikijenga ofisi za Udart eneo la Jangwani.