Mvutano wa Tanesco, makandarasi wamuibua naibu waziri

Muktasari:

  • Inadaiwa kuwa kampuni ya State Grid inailalamikia kampuni ya uzalishaji nguzo ya Qwihaya kuchelewa kufikisha nguzo za umeme kwenye maeneo yanayotakiwa kusambazwa umeme na matokeo yake, kaya zilizoomba kuunganishiwa umeme kutoungwa kwa wakati.

Morogoro. Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kumaliza mvutano kati yake na kampuni mbili zilizopewa tenda ya kusambaza umeme vijijini.

Kampuni hizo ni zile zilizopatiwa kandarasi na Wakala wa Umeme vijijini(REA) za State Grid Electrical & Technical Work limited na kampuni ya uzalishaji nguzo za umeme ya Qwihaya General Inteprices limited.

Inadaiwa kuwa kampuni ya State Grid inailalamikia kampuni ya uzalishaji nguzo ya Qwihaya kuchelewa kufikisha nguzo za umeme kwenye maeneo yanayotakiwa kusambazwa umeme.

Naibu waziri Mgalula amesema hayo leo Mei 24 katika Kijiji cha Dibamba wilayani Mvomero mkoani Morogoro, alipokuwa akikagua na kuwasha umeme katika kijiji hicho.

Amesema kuwapo kwa mgogoro wa kuvutana baina ya kampuni hizo kunachelewesha utakelezaji wa mradi huo wa umeme vijijini, jambo linalowafanya wananchi kuchelewa pia kupata huduma.

Awali, ilidaiwa kuwa mzalishaji alipeleka nguzo 2,000 lakini baada ya msimamizi ambaye ni Tanesco kufanya ukaguzi, alibaini kuna nguzo zaidi ya 900 zisizokuwa na viwango hivyo kugoma kuzitumia na kusababisha mradi huo kufanyika kwa kusuasua.

Aidha, Naibu waziri huyo ametoa muda wa wiki moja kwa Tanesco kuhakikisha inatatua mgogoro huo ili kazi hiyo iendelee kufanyika na kukamilika kwa wakati.

“Msimamizi wa mradi kutoka wizarani, Tanesco, REA, mkandarasi nataka muafaka wa changamoto zilizopo ndani ya wiki moja tupate majibu, msiposhughulikia hili mjue wanaoumia ni wananchi,” alisema.

Hata hivyo, amesema kasi ya mkandarasi si ya kuridhisha na amemtaka kutoondoka eneo la mradi hadi atakapokamilisha kuwaunganishia umeme wateja 98 waliobaki wa Kijiji cha Dibamba. Kati ya wateja 103 waliomba kuunganishiwa umeme 15 pekee ndiyo waliounganishiwa

Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mohamed Utaly amesema wilaya hiyo ina jumla ya kata 30, vijiji 130 na vitongoji 686 na mradi wa REA awamu ya pili na ya tatu, wilaya hiyo kwa awamu ya pili na tatu vijiji vitakavyonufaika ni 24.

Naye Meneja wa Tanesco Wilaya ya Mvomero, Basilius Kayombo ametaja changamoto zilizopo kuwa ni baadhi ya nguzo kushindwa kufikia viwango na zingine zinafika na kupimwa eneo la mradi, jambo ambalo si sahihi.

Amesema nguzo 300 zilizopimwa zilishindwa kufikia viwango na kusababisha mvutano kati ya mkandarasi, mzalishaji wa nguzo na wasimamizi.

“Kutokana na hilo, mzalishaji wa nguzo hataki kuchukua nguzo zilizoshindwa kufikia viwango na hata kutishia kutoleta nguzo nyingine, maelezo haya yanaharibu na kudhoofisha maendeleo ya mradi, alisema Kayombo.