Mwakilishi Zanzibar ataka vijana walipiwe mahari wakitaka kuoa

Thursday May 16 2019

 

By Haji Mtumwa, Mwananchi [email protected]

Unguja. Mwakilishi wa Ole, Mussa Ali Mussa ameunga mkono kauli ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Unguja, Ayoub Mohamed Mahmoud ya kuwataka vijana katika mkoa wake wasio na uwezo wa kifedha kulipa mahari kwa ajili ya ndoa wafike ofisini kwake ili kuwatafutia fedha hizo.

Mussa amesema hayo leo Alhamisi Mei 16 katika Baraza la Wawakilishi linaloendelea mjini Unguja, wakati akichangia hatuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara ya nchi, ofisi ya Rais, tawala za mikoa kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Amesema kitendo cha mkuu huyo wa mkoa kinahitaji kuungwa mkono na kila mmoja wakiwamo wakuu wa mikoa wengine ili kusaidia kupunguza idadi ya vijana wasio kuwa na ndoa.

“Ni wazi kwamba hatua ya kuwapa mahari vijana ni moja ya mambo ambayo yanaweza kuwa sababu kuu ya kuondoa vitendo vya ubakaji wanawake na watoto.”

“Niwaombe sana wakuu wengine wa mikoa wakiwamo wa Pemba nanyi muige mfano wa mkuu wa mkoa wa Mjini Unguja kwa kuwatangazia vijana katika mikoa yenu kuwapa mahari ili waingie katika ndoa,” amesema.

Juzi, Mahmoud katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni kisiwani hapa, aliwataka vijana walioshindwa mahari kwa ajili ya ndoa wafike ofisini kwake ili kupata msaada.


Advertisement