Mwalimu anayefundisha madarasa sita peke yake, aanza kujengewa nyumba

Wednesday March 20 2019
mwalimupic

Mtwara. Mwalimu Bosco Chilumba wa Shule ya msingi Chikotwa halmashauri ya wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara ameanza kujengewa nyumba ya miti baada ya kuishi kwenye nyumba ya kupanga kwa zaidi ya miaka minne.

Chilumba ni mwalimu pekee wa shule hiyo ambaye amekuwa akilazimika kufundisha madarasa sita kuanzia darasa la awali hadi la tano.

Hivi karibuni gazeti la Mwananchi liliibua habari ya mwalimu huyo na shule kwa ujumla hali iliyosababisha uongozi wa wilaya, mgambo kwa kushirikiana na wananchi kuanza ujenzi wa nyumba moja watakayoishi walimu watatu.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Machi 20, 2019 mkuu wa wilaya hiyo Moses Machali, amesema wameanza ujenzi wa nyumba watakayoishi walimu watatu baada ya kukamilika wataongeza walimu wawili.

“Tumeanza ujenzi  na tunategemea itakamilika ndani ya wiki mbili zijazo, tunaijenga kwa kasi lakini kwa uhakika na imara na itakapokamilika tutapeleka walimu wawili ili wawe watatu,” amesema Machali.

Pia, amesema baada ya kukamilika kwa nyumba ya walimu wataanza mchakato wa kuongeza chumba kimoja cha darasa.

Advertisement

Mwalimu Bosco ameshukuru kwa hatua zilizochukuliwa na kusema amepata faraja kubwa na nyumba hiyo itakuwa mkombozi kutokana na mazingira anayoishi kwani alikuwa akitamani kupata sehemu huru.

“Mambo ni mazuri baada ya kuanza ujenzi nimepata faraja kubwa sana na kasi yao ni kubwa mno, hii (nyumba) itakuwa ni bora zaidi ikikamilika kwa maelezo wanayosema kwa hiyo nitakuwa huru zaidi kufanya kazi na itakapokamilika nitaongezewa walimu,” amesema Chilumba.

Soma Zaidi: Mwalimu afundisha madarasa sita peke yake


Advertisement