VIDEO: Mwanafunzi wa kidato cha nne ajiua kwa risasi

Morogoro. “Ni mtoto asiyewajua wazazi wake na asiyejua kazaliwa wapi? Mtoto huyu anatamani kukiona kifo chake wakati wowote, mtu yeyote atakayesoma dayari hii ndiye atakayeandika siku ya kifo chake.”

Huo ni ujumbe aliouacha mwanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Lupanga, Jasmin Ngole aliyejiua kwa kujipiga risasi kooni na kufumua sehemu ya utosi.

Kifo chake kimeacha maswali mengi kutokana maisha aliyoishi binti huyo mwenye umri wa miaka 18 pamoja na ujumbe aliyoandika kwenye shajara (diary) yake na kumkabidhi rafiki yake waliyekuwa wakisoma naye darasa moja, Imelda Milanzi siku moja kabla ya kujiua.

Mwili wa Jasmini ulikutwa kando ya barabara nyembamba, eneo la Kola B Manispaa ya Morogoro, alfajiri ya Jumanne iliyopita huku bastola aliyotumia kujiua, mali ya Profesa Hamis Maige iliyokuwa na magazine moja pamoja na ganda la risasi vikiwa kando yake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa alisema muda mfupi baada ya tukio hilo, Profesa Maige alijitokeza na kueleza kuwa bastola hiyo ni yake na anaimiliki kihalali.

Alisema profesa huyo alishikiliwa kabla ya kuachiwa kwa dhamana na kwamba baada ya uchunguzi wa kidaktari kukamilika, mwili wa binti huyo ulizikwa katika makaburi ya Kola jana.

Miongoni mwa mambo yaliyoongeza simanzi na vilio katika maziko hayo ni hali ya Imelda aliyekuwa ameachiwa ujumbe kabla ya shoga yake kujitoa uhai. Binti huyo licha ya kushindwa kuzungumza kwa kilio mfululizo, alikuwa akipoteza fahamu mara kwa mara.

Mwalimu Neema Kambi aliyekuwa akimsaidia alisema Imelda hawezi kuzungumza chochote, “kwa sasa yuko kwenye taharuki na hofu kubwa, alikuwa rafiki yake wa karibu na ndiyo mtu wa mwisho kuonana na Jasmin, bila ya kumpa ushauri nasaha anaweza akaathirika kisaikolojia.”

Mama mlezi wa Jasmin, Christina Makinda ambaye kwa sasa anaishi Ruangwa mkoani Lindi akizungumza na Mwananchi msibani, alisema mama mzazi wa Jasmin alikuwa akifanya kazi za ndani nyumbani kwa wazazi wake (Milanzi) na alifariki dunia muda mfupi baada ya kujifungua Jasmin.

Alisema baada ya kifo hicho, alichukua jukumu la kumchukua mtoto huyo na kwenda kumlea nyumbani kwake wakati huo kiishi na Profesa Maige kama mke na mume na walipotengana alihamia Ruangwa na kumuacha Jasmin kwa profesa huyo.

Alisema Jasmin alikuwa mtoto mwenye adabu na mwadilifu lakini alibadilika tabia siku siku chache kabla hajachukua uamuzi wa kujiua akisema alikuwa akitoka nyumbani bila kuaga na kurudi usiku wa manane bila kueleza alikokuwa.

“Profesa alinipigia simu na kunieleza mabadiliko ya tabia ya Jasmin. Nilifanikiwa kuongea naye kwenye simu lakini kila nilichokuwa namuuliza alikataa, baadaye nikamwambia nitawaambia walimu kuhusu tabia yake, bado hakujibu chochote,” alisema Christina.

Alisema siku ya pili, Profesa Maige alimpigia tena simu akimweleza taarifa ya kupotea kwa Jasmin na siku iliyofuata alipigiwa na kupewa taarifa za kifo cha binti huyo.

Makamu Mkuu wa Sekondari ya Lupanga, Daud Masunga alisema kitaaluma, maendeleo ya Jasmin yalikuwa ya wastani lakini alikuwa mwanafunzi mcheshi, mwenye nidhamu na aliyekuwa na ushirikiano mzuri na wanafunzi wenzake.

Mwalimu Masunga alisema hajawahi kupokea malalamiko kutoka kwa walezi wake wala wanafunzi wenzake kuhusu mienendo yake ya kitabia hivyo kifo hicho kimewaachia maswali mengi na hofu kwa wanafunzi wenzake.

Mmoja wa wanafunzi wa kidato cha nne aliyekuwa akisoma na Jasmin, Dafrosa Wilfred alisema siku moja kabla ya kujiua, Jasmin alionekana kuwa na furaha iliyopita kiasi na alikuwa akizungumza na kufurahi na kila mwanafunzi.

Dafrosa alisema Jasmin hakuwahi kuwaeleza hali ya maisha anayoishi wala hakuonekana kama ni mtu mwenye matatizo ya kimaisha kwa sababu alikuwa akipata kila mahitaji yaliyokuwa yakihitajika shuleni kutoka kwa walezi wake.

Akimzungumzia binti huyo, Zakia ambaye ni mmoja wa mabinti wa Profesa Maige alisema waliishi na Jasmini kwa upendo na alipokuwa akikosea walikuwa wakimuonya kama ndugu yao.

Alisema taarifa alizozipata baada ya tukio hilo zinaeleza kuwa siku moja kabla ya kujiua, Jasmin alionekana akiwanunulia vyakula na vitu vidogo wanafunzi wenzake huku akiwaambia kwamba hiyo ni siku yake ya mwisho kuishi hapa duniani hivyo kila mmoja ale anachokipenda.

Alisema hawezi kujua namna Jasmin alivyofahamu mahali ilipokuwa bastola ya Profesa Maige katika nyumba yao iliyokuwa na watu wanne.