Mwanamke ajidunga sindano yenye matunda

Muktasari:

  •  Sindano hiyo inadaiwa kuwa na mchanganyiko wa matunda zaidi ya 20 ambayo ilimletea madhara kwenye Ini,figo na mishipa ya damu

Xiangnan ,China.Mwanamke mmoja nchini China amenusurika kifo baada ya kujidunga yeye mwenyewe sindano iliyosheheni mchanganyiko wa matunda yaliyotengenezwa kwa jitihada za kuwa na afya.

Baada ya kujidunga sindano hiyo Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 51,alijisababishia madhara kwenye ini, figo, moyo na uharibifu wa mapafu.

Hivyo alilazimika kuwekwa kwenye cha uangalizi maalumu (ICU) kwa muda wa siku tano.

Sindano hiyo ilikuwa na mchanganyiko wa matunda tofauti zaidi ya ishirini aliyojidunga kwenye mishipa ya damu.

Taarifa hii ni kwa mujibu wa mfanyakazi mmoja aliyeko katika Hospitali yenye ushirika na Chuo Kikuu cha Xiangnan kilichoko mjini Hunan alipozungumza na Shirika la Habari la BBC.

Watumiaji wa mitandao nchini China wanadai kwamba tukio la mwanamke huyo limeibua hisia na uhitaji wa ufahamu wa huduma ya kwanza kwa jamii.

Inaarifiwa kuwa baada ya kujidunga mchanganyiko huo wa matunda, mwanamke huyo ambaye jina lake limehifadhiwa, alianza kujihisi ngozi yake inauma na kugeuka kuwa nyekundu, na joto likawa likiongezeka mwilini mwake.

Baada ya hali hiyo, alipokwenda hospitalini ikamlazimu kulazwa katika kitengo cha wagonjwa mahututi Februari 22, kabla ya kuhamishiwa katika hospitali kuu na baadaye kuruhusiwa.

Tukio hilo limezua mjadala na kugeuka kuwa gumzo nchini China,mitandao ya kijamii ikiwemo mtandao wa kijamii wa Weibo. Zaidi ya watu elfu kumi na mmoja wa mtandao huo walitumia msemo huu #OldWomanPutsJuiceIntoVeins.

Mtu mmoja alinukuliwa akisema inaonekana kwamba ''ujuzi wa matibabu wa umma bado ni mdogo sana."