Mwanamke anayeendesha maisha kwa kuendesha gari la kubebea maiti

Moshi. Wapo wanawake wengi pengine hata wanaume, ambao huogopa maiti na wengine hata kuisogelea ni shida, lakini si Grace Mcha.

Mama huyo amechagua kuwa dereva wa gari za kubeba maiti kazi ambayo imemfanya kuwa mashuhuri mjini hapa. Kila anapoonekana katika shughuli mbalimbali za mazishi, watu wamekuwa wakijiuliza maswali mengi juu ya ujasiri wake wa kubeba miili ya marehemu, kazi inayoogopwa si na wanawake wenzake tu, bali watu wengi.

Grace, ambaye ni dereva katika kampuni ya God Mark Funeral Directors, anasema hata siku ya kwanza kuanza kubeba jeneza lenye mwili, hakuwahi kuota wala kulala usingizi wa mang’amng’amu.

Kampuni ya God Mark Funeral Directors ya mjini Moshi, ndio ambayo mwaka jana ilitangaza kutoa vifurushi vya mazishi ikiwamo punguzo la asilimia 30 kwa atakayenunua jeneza lake akiwa hai.

Siku ya kwanza kubeba maiti

Mwanamke huyo ambaye anaonekana kama tofauti na pengine baadhi ya watu kumshangaa kwa kazi yake hiyo, aliajiriwa na kampuni hiyo Aprili mwaka jana.

Grace anafahamu kwamba wapo watu wanaoogopa hata kugusa maiti tu, lakini yeye anasema ana hofu ya Mungu tu na anafahamu kwamba kifo kimeumbiwa mwanadamu hivyo haikumpa shida alipoanza kazi hiyo.

“Wapo ambao wakiona maiti pengine hawapati usingizi au hata wakilala wanalala usingizi ni wa mang’amung’amu lakini huwezi kuamini. Siku ya kwanza naanza kubeba maiti wala sijawahi hata kuota kwa sababu nina hofu ya Mungu na ninajua kifo kimeumbiwa mwanadamu na sisi sote tutakufa,” alisema.

“Leo nikianza kuogopa mtu aliyekufa hivi mimi kesho au kesho kutwa au mtondogoo nikifa itakuwaje? Watu wote wakiniogopa au wakinihofia maana yake sitazikwa? Kwa kweli sijawahi kuota”.

Uzoefu wa kuendesha magari

Mwanamke huyo anasema kati ya mwaka 1989 na 1990 alikwenda New Zealand alikoishi kwa takribani miaka miwili. Akiwa huko aliingia kwenye shule ya udereva baada ya kupata kibarua.

“Nilipata kazi ya kusambaza matunda na ni lazima niwe naendesha gari mwenyewe kusambaza bidhaa. Nilienda shule ya udereva na kufuzu,” alisema mwanamke huyo na kuongeza:

“Nilirudi nyumbani 1992 na ilipofika mwaka 2000 nilienda kuomba kazi ya ofisa mauzo kwenye kampuni ya mikate ya Baba Loaf nikaendesha gari kama sales woman (afisa mauzo)”.

“Mwaka 2006 ilitokea kazi Muwsa (Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi) za udereva. Nimeendesha kwa miaka 11 hadi 2017 nilipunguzwa kazi pale.

“Kabla ya kuja God Mark nilikuwa dereva wa mabasi makubwa ya kampuni ya Ibra Line kutoka Dar es Salaam hadi Masasi kupitia Mtwara na Lindi. Abiria wangu wananifahamu sana.”

Kuhusu kazi yake ya sasa alisema, “niliona nitoke na fani tofauti na wamama wengine ambao pengine wanapenda kazi za kuajiriwa maofisini. Niliamua nitoke kama mwanamama niwe mfano kwa kutochagua kazi.“Kutokana na nature (asili) ya kazi yenyewe niliamua kuvaa ujasiri. Watu wanaona ni kazi inayotisha lakini mimi naona ni kazi kama kazi nyingine inayotakiwa uwe na huruma”

“Ni kazi yenye changamoto lakini ukishatambua hawa ni wafiwa, basi haina shida. Wanaweza kukuambia njoo saa 12 asubuhi, lakini wao wakaja saa mbili au saa tatu. Inabidi uwe mvumilivu”.

Matukio anayoyakumbuka

Grace anasema tangu aanze kazi katika kampuni hiyo, anakumbuka matukio mawili makubwa, ambayo kwake anaona yalikuwa changamoto.

“Tukio la kwanza nilienda Tukuyu kule mpakani mwa Malawi na Tanzania kupeleka mwili wa binti wa miaka 20. Ndio alikuwa mtoto wa pekee katika hiyo familia,” anasema Grace na kuongeza;

“Mzazi (mama) alikuwa analia sana kwa sababu ni mtoto wa pekee. Ule uchungu wa mama uliniumiza sana mimi kama mwanamke. Nilipata wakati mgumu sana. Nilijikaza sana siku ile”

“Tukio lingine nilienda KIA kuchukua mwili. Ndio ilikuwa mara ya kwanza kupokea mwili. Kuna kijana alifariki Namibia. Kuna taratibu nyingi sana za kufuata pale. Kwanza ile utaratibu wa clearance (kutoa) ilikuwa shughuli kubwa kwangu kwa siku ile. Namshukuru Mungu maana ilikuwa siku ngumu kwangu lakini nilifanikisha nikaleta mwili Machame Hospitali”.

Ushauri kwa wanawake wenzake

“Niwashauri wanawake wenzangu waache kuwa na fikra potofu kuwa kuna kazi ya mwanamume na kuna kazi ya mwanamke,” anasema Grace, “hakuna sehemu iliyoandikwa hii ni kazi ya mwanamke na hii ni kazi ya mwanamume. Ndio maana mimi nimeendesha mabasi ya abiria tena umbali mrefu tu. Ni wanawake wa kuwahesabu. “Ukijiamini, ukijitambua na kujielewa, kazi yoyote unaweza kufanya. Ni kweli hii kazi hata wapo wanaume wanaiogopa lakini ukitizama sana ni hofu ambayo huna sababu ya kuwa nayo.”

Grace anasema kutokana na changamoto ya ajira kwa sasa, wanawake hawapaswi kuchagua kazi za kuajiriwa maofisini tu, hata ikibidi wajitose kwenye kazi ambazo hawajazizoea.

Mwanamke huyo alizaliwa mwaka 1971 huko Babati na ni mtoto wa pili kwa wazazi wake. Ni mama wa watoto wawili wa kiume ambaye anasema anaishi maisha ya kawaida.