Mwanamke wa bodaboda anayetamani malori

Saturday March 16 2019

Cesilia Paul akiwa amepakia abiria kwenye

Cesilia Paul akiwa amepakia abiria kwenye bodaboda anayoendesha. Picha na Ngollo John 

By Ngollo John, Mwananchi [email protected]

Mwanza. “Natamani siku moja nije kuendesha gari kubwa la mizigo kama malori au semi-trela.”

Hiyo ni kauli ya Cesilia Paulo (34), mkazi wa Mtaa wa Nyasaka ‘A’ wilayani Ilemela ambaye kwa sasa anaendesha pikipiki maarufu bodaboda.

Zamani ilizoweleka kwamba kazi hiyo ilikuwa ikifanywa na wanaume, lakini hivi sasa ili mkono uende kinywani hata akinamama wameanza kuifanya.

Cesilia ambaye ni mama wa watoto wanane anasema alianza kazi hiyo 2016 baada ya kuambiwa na mumewe kuwa inalipa.

Anasema yeye na mume wake, Noberth Gabriel ni waendesha bodaboda ambao kwa sasa wanasomesha watoto wao mmoja akiwa kidato cha tano.

“Ni kazi yenye risk (hatari) hasa kwetu wanawake, lakini hatuna budi kuifanya ili kuweza kujipatia kitu chochote cha kulisha familia,” anasema Cesilia aliyehitimu elimu ya msingi 1999.

Anasema kabla ya kuingia kwenye shughuli hiyo alikuwa akiuza samaki wa kukaanga ambao anadai walikuwa hawamlipi.

Baadaye alianza kujaza mchanga kwenye malori kwa kipindi cha miaka sita kuanzia 2009 hadi 2015 kabla ya kuwa dereva wa bodaboda

Alijifunzaje pikipiki?

“Baada ya makubaliano, Noberth (mumewe) alianza kunifundisha kuendesha zoezi nililolifanya kwa kipindi cha miezi mitatu kisha akaninunulia pikipiki aina ya SLG,” anasema.

Anasema mwanzo wakati anaanza kazi hiyo alikuwa anabaguliwa hasa na wanawake wenzake wakihofia kuangushwa. Hata hivyo baada ya muda alizoweleka, ingawa changamoto iliyofuata ilikuwa ni ile ya kushikwa kiuno na abiria.

“Nilimuuliza mume wangu kwa nini abiria wananishika kiunoni? Alinieleza kuwa ni kawaida hata wao (wanaume) hushikwa hivyo hivyo, ndio nikapata moyo wa kuendelea na shughuli.”

Familia, mafanikio

Cesilia anasema kila siku huamka saa 10 alfajiri kuingia barabarani na baada ya hapo hurejea nyumbani kuwaandaa watoto waende shule.

Anasema watoto wanapoondoka hurudi tena barabarani ambapo hufanya kazi hadi saa sita mcha kisha hurudi nyumbani kupika chakula cha mchana.

Mama huyo anasema kabla hawajaanza kazi hiyo na mumewe walikuwa hawajajenga nyumba ya kuishi, lakini hivi sasa wamejenga pamoja na nyingine yenye vyumba vitatu ya wapangaji.

Kwa siku, anasema huingiza kati ya Sh15,000 hadi 20,000 ambazo humsaidia kuendeshea maisha.

Cesilia anasema kuna watu wanampongeza kwa kazi anayofanya, lakini wapo pia wanaomkebehi kuwa siyo kazi nzuri.

“Asilimia kubwa ya abiria ninaowabeba ni wanaume, wanawake baadhi yao hawanipendi na wengine wanaogopa kuwa nitawaangusha.”

Matamanio yake

Cesilia anasema anatamani kuwa dereva anayeendesha magari makubwa kama malori.

Anasema endapo atapata mfadhili wa kumpeleka kusomea udereva anaweza kufanya kazi hiyo.

“Nilishazungumza na mume wangu kuhusu hilo jambo, alikubaliana na mimi ila kwa sasa hana uwezo wa kunipeleka chuo cha udereva ili nipate leseni ya kuendesha hayo magari makubwa, hivyo ni ombi langu endapo mtu akipatikana niko tayari kufanya kazi hiyo,” anasema.

Mumewe anasemaje?

Noberth Gabriel (48), mume wa Cesilia anasema kabla mkewe hajaanza kazi hiyo alikuwa anategemewa yeye kwa kila kitu na familia.

Anasema, aliamua kumshawishi na kumfundisha kuendesha pikipiki ili wasaidiane.

Noberth anayeegesha bodaboda yake eneo la Kiloleli wilayani Ilemela, anawasihi wanaume wenzake kuwapatia nafasi wake zao wafanye vitu wanavyovipenda.

Anasema katika dunia ya sasa majukumu ya familia hayawezi kuelekezwa kwa mtu mmoja pekee.

Advertisement