Mwananchi kinara kuripoti habari zenye vyanzo vingi

Muktasari:

  • Matokeo ya utafiti wa ubora wa maudhui ya vyombo vya habari Tanzania kwa mwaka 2018 unaonyesha kwamba ubora wa maudhui umeshuka kwa kuzingatia vigezo vya kitaaluma, utimilifu wa habari, kueleweka kwa habari na maadili.
  • Jumla ya machapisho 1,886 yalipitiwa katika utafiti huo yakiwemo machapisho ya magazeti 560, habari na vipindi vya redio 433, habari na vipindi vya televisheni 243 na blogu/mitandao 159.


Dar es Salaam. Matokeo ya utafiti wa ubora wa maudhui ya vyombo vya habari Tanzania kwa mwaka 2018 yamebainisha kuwa vyombo vingi kutoripoti habari zitokanazo na wao wenyewe badala yake vinategemea habari za matukio.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo ulioandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) leo Ijumaa Februari 15,  2019 mtafiti, Christoph Spurk amesema ni asilimia 36 tu ya vyombo vya habari vinakuwa na vyanzo vya habari zaidi ya kimoja huku gazeti la Mwananchi likiongoza kwa asilimia 86 na kufuatiwa na Nipashe kwa asilimia 66.

Utafiti huo umebainisha kwamba vyombo vingi vinaripoti habari kwa chanzo kimoja cha habari, havitumii wanawake kama vyanzo vya habari na haviripoti ukosoaji wa Serikali.

Kuhusu habari za kuikosoa Serikali, Spurk amesema Jamii Forum inaongoza kwa asilimia 35 na kufuatiwa na kituo cha radio cha Pangani FM kilichopata asilimia 15 wakati vyombo vingine vikiwa na viwango vya chini zaidi.

Utafiti huo unabainisha kwamba vyombo vya habari vinavyoripoti habari ambazo vyanzo vyake ni wanawake pia vimeshuka, gazeti la Jamhuri likiwa na asilimia 16 wakati Mwananchi ikiwa na asilimia 8.

Kwa upande wa kuripoti habari zenye mitazamo tofauti ndani ya habari, utafiti umebainisha kushuka kwa kiwango hicho huku magazeti ya Jamhuri na Daily News yakifanya vizuri katika eneo hilo kwa asilimia 30 na kufuatiwa na Zanzibar Leo kwa asilimia 15.

Akiwasilisha mapendekezo katika utafiti huo, mtafiti Abdallah Katunzi ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amesema vyombo vya habari na waandishi wa habari waandae sera ambayo itasaidia kuongeza idadi ya habari zitokanazo na wao wenyewe kwa lengo la kupunguza idadi ya habari za matukio.

"Vyombo vya habari visiripoti habari tu, bali wahakikishe wanaripoti habari hizo kwa kuweka mitazamo mbalimbali ndani yake huku wakiongeza usuli wa habari na kueleza kwa nini wanaripoti habari hizo," amesema Katunzi.

Katunzi amependekeza kwamba vyombo vya habari kutoa mafunzo kwa waandishi na wahariri kwa kuzingatia maeneo ambayo hawakufanya vizuri. Amesema mafunzo hayo yatolewe pia kwa waandishi waliopo mikoani.