Mwananyamala, Kijitonyama zinavyotisha kwa uzalishaji takataka

Muktasari:

Kama wewe ni mkazi wa Mwananyamala, Kijitonyama au Makumbusho, basi fahamu kwamba kata yako ni moja kati ya kata zinazoongoza katika uzalishaji wa takataka kwa wingi zaidi kuliko kata nyengine yoyote katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Dar es Salaam. Kama wewe ni mkazi wa Mwananyamala, Kijitonyama au Makumbusho, basi fahamu kwamba kata yako ni moja kati ya kata zinazoongoza katika uzalishaji wa takataka kwa wingi zaidi kuliko kata nyengine yoyote katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya halmashauri hiyo (municipal profile) ya mwaka 2017 ambayo imewekwa katika tovuti yake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Manispaa ya Kinondoni, ambayo kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 ina wakazi wapatao 929,681, inakadiriwa kuzalisha takataka takribani tani 1,223.6 kwa siku (ambazo ni sawa na tani 446,614 kwa mwaka).

Kati ya kata ishirini zilizopo katika manispaa hiyo, Mwanayamala inaongoza kwa kuzalisha takataka nyingi zaidi ambapo kwa kila siku huzalisha jumla ya tani 108.5. Kata za Makumbusho na Kijitonyama zinafuatia kwa kila moja kuzalisha jumla ya tani 103.5 na 101 ya takataka kwa siku.

Wakazi wa Manispaa ya Kinondoni, yenye jumla ya mitaa 106, wanaoweza kutembea kifua mbele kwa kuzalisha takataka kwa kiwango kidogo kabisa kuliko kata zote ni wale wa Mbweni, Mabwepande na Bunju. Kila moja kati ya kata hizi huzalisha tani 11.4, 12.4 na 20 kwa siku.

Ni vigumu kufahamu ni kwa nini haswa Mwananyamala, Kijitonyama au Makumbusho zinaongoza kwa kuzalisha taka taka nyingi wakati Kata za Mbweni, Mabwepande na Bunju zinazalisha takataka kwa kiwango cha chini kabisa.

Ukijaribu kuichambua kwa makini taarifa hiyo unaweza ukasema kwamba pengine idadi ya watu na mitaa ya kata husika huchangia uwezo wake wa uzalishaji takataka.

Kwa mfano, wakati Mwananyamala ina jumla ya wakazi wapatao 64,529 na mitaa nane, Mbweni ina wakazi 42,050 na mitaa mitano tu.

Lakini dhana hiyo inabatilishwa kwa kulinganisha Kata za Kijitonyama na Mabwepande. Wakati Kijitonyama ina wakazi 74,193 na mitaa saba, Mabwepande ina wakazi 76,878 na mitaa mitano. Vivyo hivyo, wakati kata ya Makumbusho ina wakazi wapatao 32,494 na mitaa sita, Bunju ina wakazi 62,436 na mitaa sita.

Abilu Peter, ambaye ni ofisa usafi na mazingira katika Halmashauri ya Kinondoni, anasema idadi ya watu na mitaa inaweza kuwa kigezo kwa kiasi fulani lakini haiwezi kuelezea picha nzima ya tatizo lenyewe.

“Unajua kuna suala la tabia na hulka pia za baadhi ya wananchi wa kata hizi, hususani katika suala la utumiaji wa vifungashio,” anasema Abilu.

“Maeneo ambayo watu wake wanapenda sana kutumia vifungashio hata kwa vitu vidogo tu – kama vile mifuko ya plastiki – ni lazima uzalishaji wao wa takataka utakuwa mkubwa ukilinganisha na zile ambazo wakazi wake hawana hulka hizo.”

Kata nyengine zilizopo katika halmashauri hiyo na uwezo wao wa kuzalisha takataka kwa siku na kwa tani ni Mikocheni (84), Kunduchi (88), Msasani (92), Hananasif (74) na Kinondoni (55).

Nyingine ni Kawe (62), Mbezi Juu (50), Makongo (50), Wazo (40), Magomeni (36), Ndugumbi (38), Kigogo (51.4) na Mzimuni (51.4).