Mwananyamala yakwaza wazazi

Muktasari:

  • Mmoja wa wahudumu anayehusika kutoa huduma hiyo ambaye jina lake halikufahamika alisikika akiomba radhi na kusema ubovu wa vifaa unachangia kuchelewesha huduma hiyo.

Dar es Salaam. Wanawake waliojifungua katika hospitali ya Mwananyamala wamelalamikia utaratibu uliowekwa hospitalini hapo wa kupata matangazo ya watoto wao wakisema unawakwaza.

Mwananchi jana ilifika katika ofisi ya uzazi na vifo hospitalini hapo na kukuta tangazo jipya mlangoni lililoandikwa “Kuanzia tarehe 21 (juzi) kutakuwa na utaratibu wa kutoa matangazo kwa watu arobaini kila siku kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi 5:00 asubuhi”.

Mkazi wa Kinondoni Ashura Issa alisema wameshangazwa na utaratibu huo kwani wanaoishi mbali watakosa huduma hiyo kwa kuwa wengi wao watashindwa kujihimu asubuhi kutokana na umbali wa maeneo wanayoishi.

“Zamani haya mambo hayakuwapo ilikuwa unakuja unajifungua na siku ya kuondoka unapewa tangazo lakini sasa kwakweli kila mtu amepatwa na hasira siyo siri wamenikatisha tamaa ya kufuatilia.”

“Tulikuja hapa jana tukaambiwa tuandike majina yetu kisha turudi Januari 29, lakini pia kuna ambao waliandika majina yao jana wakaambiwa watapatiwa leo lakini hawakupata,”alisema.

Mkazi wa Gongo la Mboto, Lucy Meckson alisema tangu ameanza kufuatilia tangazo la mwanae ni wiki ya tatu sasa hajafanikiwa.

Mmoja wa wahudumu anayehusika kutoa huduma hiyo ambaye jina lake halikufahamika alisikika akiomba radhi na kusema ubovu wa vifaa unachangia kuchelewesha huduma hiyo.

Ofisa utumishi hospitali, hiyo, Mansor Karama alisema huenda huduma hiyo ikawa inasusua kutokana na uchache wa watumishi.