Mwandishi wa habari Dw afariki

Muktasari:

Mwenyekiti wa APC, Claud Gwandu alisema jana kuwa Ngereza alifariki akiwa anapatiwa matibabu baada ya kuugua ikiwa ni siku chache tangu aliporejea nchini kutoka nchini India kwa matibabu.

Arusha. Mwandishi wa habari mwandamizi wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio Deutsche Welle ya Ujerumani (Dw), Charles Ngereza (pichani) amefariki dunia baada ya kusumbuliwa na matatizo ya ini.

Ngereza ambaye pia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Arusha (APC), alifariki jana asubuhi akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali teule ya wilaya ya Arusha ya St Elizabeth.

Mwenyekiti wa APC, Claud Gwandu alisema jana kuwa Ngereza alifariki akiwa anapatiwa matibabu baada ya kuugua ikiwa ni siku chache tangu aliporejea nchini kutoka nchini India kwa matibabu.

“Taratibu za mazishi zinafanyika nyumbani kwa marehemu eneo la kwa Mrefu katika jiji la Arusha,” alisema Gwandu.

Ngereza kabla ya kujiunga na Dw alikuwa mwandishi wa Radio One na gazeti la Nipashe mkoani Arusha na ameacha mke na watoto.