Mwandosya ashukuru kung'oka Chuo Kikuu Mbeya

Dar es Salaam. Profesa Mark Mwandosya amezungumzia kuondolewa kwenye nafasi yake ya ukuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya, akisema ingawa alipaswa kumaliza mwaka 2020, bado anashukuru na kumpongeza aliyechukua nafasi yake.

Jana (Alhamisi Desemba 6), Rais John Magufuli alitangaza uteuzi wa nafasi mbalimbali, huku akimteua makamu mwenyekiti wa zamani wa CCM, Pius Msekwa kuwa mkuu wa chuo hicho badala ya Mwandosya.

Baada ya uteuzi huo mpya, Profesa Mwandosya aliyetangaza kupumzika siasa, aliandika kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter akimpongeza Msekwa kwa kumpokea kijiti na kukishukuru chuo hicho kwa ushirikiano waliompa.

“Aprili 2014  Kikwete aliniteua mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya kwa kipindi kinachoishia 2020. Mheshimiwa Pius Msekwa anachukua nafasi hiyo kuanzia leo. Nampongeza. Nashukuru kwa heshima ya kuwa mlezi mkuu wa chuo,” ameandika Profesa Mwandosya.

Hivi karibuni pia, Mwandosya aliondolewa katika nafasi ya Uenyekiti wa bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere(MNMA) na nafasi yake kuchukuliwa na waziri na mbunge wa zamani wa Bunda, Steven Wassira.

Baada ya mabadiliko hayo, Profesa Mwandosya aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter akilezea shukrani zake huku akimnukuu Mwalimu Julius Nyerere kuwa alifundisha kushukuru kwa fursa yoyote unayopewa katika utumishi wa umma.