Mwekezaji ampinga mbunge mgogoro wa uwekezaji Ngara

Mbunge wa jimbo  Ngara mkoaani Kagera Alex Gashaza akiwa chini ya ulinzi wa jeshi la polisi  kwenye mkutano wa kijiji  cha Kazingati  wilayani ngara baaa ya kuzomewa na wananchi alipokuwa akipinga utaratibu uliotumika kuwapatia ardhi wawekezaji kutoka Korea kusini  wananchi .Picha na Maktaba

Ngara. Mwakilishi wa mwekezaji kutoka Korea Kusini, Issa Husein Samma aliyeko wilayani Ngara, Kagera ameibuka kupinga hoja za mbunge wa Ngara, Alex Gashaza anayedai taratibu za kupata ardhi ya uwekezaji zilikiukwa.

Samma alisema tangu kuanza taratibu za kuomba ardhi alikuwa akifanya ufuatiliaji wa karibu katika halmashauri ya wilaya ya Ngara na kwamba mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo aliomba ardhi kila kijiji eka 100.

Alisema halmashauri ilipotoa barua kwa vijiji 72, kijiji cha Kazingati kilitoa eka 50 kwa mujibu wa sheria na halmashauri ingetoa eka 100 na kiasi kingine kingeidhinishwa na kamishna wa ardhi kwa niaba ya Rais.

Alisema ardhi iliyopo kijiji cha Kazingati ni zaidi ya eka 8,000 hivyo halmashauri ya wilaya ya Ngara ilisaini mkataba (MOU) wa kuridhia uwepo wa eka 12,000 wakitegemea kupata kibali kutoka kwa kamishna wa ardhi nchini.

Alisema wawekezaji hawawezi kupewa ardhi yote hiyo labda kama ni Watanzania, wawekezaji wa kigeni wanapata ardhi kupitia kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kudhamini halmashauri ya wilaya ya Ngara kumpatia Mwekezaji.

“Suala la ardhi linakwenda kisheria, na sheria inakwenda kiutaratibu ambapo kijiji kina nafasi yake wilaya inayo nafasi na Taifa kwa ujumla kwa raia wa kitanzania na raia wa kigeni katika wawekezaji wa ndani na watokao nje ya nchi,” alisema.

Alisema kijiji cha Kazingati kilitoa ardhi ekari 50, na mkataba ulisainiwa kabla ya ardhi ekari 12,000 kupatikana isipokuwa ekari 9,000 kutoka maeneo ya kitongoji cha Musalasi na Muko ikitegemewa nyingine kutoka vitongoji jirani.

“Suala la ardhi linakwenda kisheria, na sheria inakwenda kiutaratibu ambapo kijiji kina nafasi yake wilaya inayo nafasi na Taifa kwa ujumla kwa raia wa kitanzania na raia wa kigeni katika wawekezaji wa ndani na watokao nje ya nchi,” alisema

Alisema kwamba wawekezaji hawawezi kupewa ardhi yote hiyo labda kama ni Watanzania, wawekezaji wa kigeni wanapata ardhi kupitia kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kudhamini halmashauri ya wilaya ya Ngara kumpatia Mwekezaji

Pia alisema mkutano mkuu wa kijiji ulifanyika wa kuridhia ardhi ya kijiji kutolewa kwa mwekezaji wa Korea Kusini na yeye alihudhuria na viongozi wa usalama pamoja na mkuu wa wilaya aliyewakilishwa na katibu tarafa ya Rulenge.

Aliongeza kwamba anayo barua ya kupatikana eka 50 na mwekezaji ataanzisha kilimo cha kahawa na mpunga lakini atajenga kiwanda cha mbolea na wananchi watapata fursa za mapato kujikwamua kiuchumi na kujiongezea ajira.

“Mgogoro huu ni masuala ya kisiasa maana mimi na Mbunge tuko mahasimu hivyo anapoona nasimamia anaumia lakini miradi ya wawekezaji itasaidia wananchi na wilaya kwa ujumla,’’ alisisitiza Samma

Katika hatua nyingine mwakilishi huyo amesema idara ya ardhi na mazingira wanawajibika kumpatia masharti mwekezaji atakayeingia wilayani humo kuhakikisha anatunza mazingira na analinda vyanzo vya maji.

Wananchi Wazungumza

Baadhi ya wananchi wa wilaya ya Ngara wamekuwa na maoni tofauti juu ya uwekezaji, wengi wao wakidai ni fursa ya kuwapatia ajira kwa maana kila mwenye ujasiriamali atajiongezea mapato kwa kuuza bidhaa mbalimbali zitakazohitajika.

Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) wilayani Ngara Kenedy Staford ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema wilayani humo amesema uwekezaji ni sera ya Rais na chama Tawala kuijenga Tanzania yenye uchumi wa kati na kukua kwa viwanda.

Alisema katika uwekezaji huo wananchi watapata fursa ya kujipatia ajira kwa kutumia taaluma ya fani mbalimbnali lakini hata wajasiriamali watazalisha mazao ya chakula na biashara kwa watu watakaokuwa katika miradi ya kiuchumi.

“Wananchi hasa wafanya biashara, wakulima na wafugaji kwa wilaya yetu wameanza kupewa elimu ya fursa za uwekezaji katika kata za Mugoma, Kabanga Ngara mjini na Rulenge bado Mursagamba, Benako na Rusumo,” Alisema Staford.

Maelezo ya mwenyekiti huyo wa TCCIA yalikuwa sanjari na ya aliyekuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kagera na mbunge mstaafu wa jimbo la Ngara, Pius Ngeze ambaye alisema anayepinga wawekezaji kupata ardhi anampinga Rais na chama kilichopo madarakani.

Ngeze yeye aliwataka maofisa biashara na viwanda wilayani Ngara kuwaandaa wananchi kuupokea uwekezaji na kwamba maeneo ya kuwekeza kwa wilaya ya Ngara yanapatikana tarafa za Rulenge na Mursagamba

Diwani wa Kanazi, Mathias Mugatha alikubaliana na wananchi wa kijiji cha Kashinga kuhitaji wawekezaji na kwamba mbunge anatakiwa kutumia hoja yake kwa ustaarabu bila kutofautiana na viongozi wenzake wilayani humo.

Kiongozi CCM atoa kauli

Hata hivyo Mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Ngara George Lubagola alisema mgogoro wa uwekezaji wilayani humo umekuwa gumzo katika kila kijiji hivyo wiki ijayo kamati ya siasa ya wilaya itakaa kulitolea matamko kwa watendaji serikalini.