Mwenge kuzindua miradi 62 mkoani Mara

Mkuu wa mkoa wa Mara Adam Malima ( katikati) akipokea mwenye wa uhuru kutoka kwa Mkuu wa mkoa wa Simiyu? Anthony Mtaka Leo Mei 28 katika kijiji cha Serengeti wilayani Bunda mkoani Mara.picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

Miradi 62 yenye thamani ya zaidi ya Sh31.1 bilioni inatarajiwa kuzinduliwa, kukaguliwa na kuwekewa mawe ya msingi mkoani Mara katika mbio za mwenge wa uhuru

 


Bunda. Miradi 62 yenye thamani ya zaidi ya Sh31.1 bilioni inatarajiwa kuzinduliwa, kukaguliwa na kuwekewa mawe ya msingi mkoani Mara katika mbio za mwenge wa uhuru.

Miradi hiyo ni ya sekta ya elimu, maji, kilimo, afya, utalii, ujenzi, ustawi wa jamii, viwanda na biashara na ajira  itatembelewa na mbio hizo  katika halmashauri tisa za mkoa wa Mara kuanzia leo Jumanne Mei 28, 2019.

Akizungumza katika kijiji cha Serengeti wilayani Bunda leo wakati akipokea Mwenge huo kutoka Mkoa wa Simiyu, mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima amesema katika mbio hizo kutakuwa na kumbukumbu maalumu ya Julius Nyerere.

“Mbali na kuwasha Mwenge wa Mwitongo kijijini Butiama, pia tunatarajia kufanya kumbukumbu ya Nyerere, muasisi wa mwenge wa uhuru nchini,” amesema Malima.

Katika makabidhiano hayo mkuu wa Mkoa wa Simiyu,

Anthony Mtaka amesema mkoani kwake mwenge huo umezindua miradi 34 yenye yenye thamani ya Sh8.5 bilioni.

Mtaka amesema kuwa mradi mmoja ulikataliwa kutokana na kutokukidhi viwango.