Mwenyekiti Bavicha adaiwa kutoweka tangu Januari 6

Friday January 11 2019

By Aurea simtowe,Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) jimbo la Ilala, Michael Kapamba ametoweka nyumbani kwake tangu Januari 6, 2019.

Kapamba anadaiwa mara ya mwisho aliagana na marafiki zake siku hiyo saa tatu usiku kuwa anarejea nyumbani baada ya kumaliza shughuli zao za kila siku katika soko la samaki Feri jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na  Mwananchi leo Ijumaa Januari 11, 2019 Katibu wa Bavicha jimbo la Ilala, Gerva Lyenda amesema licha ya kuagana na rafiki zake kuwa anaelekea nyumbani lakini hakufika.

“Hatujui alipo na tumetoa taarifa kituo cha polisi cha kati kwa ajili ya kuomba usaidizi wa wenzetu ili tuone wanatusaidia vipi,” amesema Lyenda.

“Kapamba ni mkazi wa Tandika na anaishi na mdogo wake ambaye pia ni mfanyabiashara katika soko la samaki feri na siku hiyo walikuwa wote ila huwa wanatofautiana muda wa kurudi na kutoka nyumbani na mara nyingi mkubwa huwa anachelewa.”

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alipoulizwa juu ya kutoweka kwa kijana huyo amesema hajasikia taarifa hizo.

"Kama taarifa ilitolewa kituoni mimi nitakuwa sina taarifa  na ndio nasikia kutoka kwako,” amesema Mambosasa.

 


Advertisement