Mwenyekiti Meru amtetea Joshua Nassari

Friday March 15 2019

 

By Happy Lazaro, Mwananchi [email protected]

Arusha. Mwenyekiti wa halmashauri ya Meru, Nelson Mafie amesema wao kama halmashauri wamesikitishwa na uamuzi wa Bunge kumvua ubunge mbunge wao, Joshua Nassari.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Machi 15, 2019 Mafie amesema mbunge huyo alikuwa akihudhuria vikao vyote vya baraza katika halmashauri hiyo bila kukosa na pindi alipokuwa na udhuru alikuwa akituma taarifa kwa maandishi.

Mafie amesema katika kipindi hicho ambacho Bunge limesema hakuhudhuria kikao cha mwezi wa tisa, si za kweli kwani mbunge huyo alionekana bungeni na alichangia hoja ya korosho.

"Ninachojua mimi Nassari vikao ambavyo alikuwa hahudhurii alikuwa anatuma taarifa tena kwa maandishi, maana huku kwetu hajawahi kukosa kikao chochote bila kuandika barua kwa maandishi," amesema.

Wakati huo huo, Nassari kesho Jumamosi anatarajiwa kuzungumza na waandishi wa habari kuelezea kilichotokea.

Habari kutoka ndani ya ofisi ya mbunge huyo zimeeleza kuwa Nassari atakuwa pamoja na viongozi wa Jimbo hilo.

Hatua ya Nassari kuzungumza inatokana na agizo alilopewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alilolitoa leo Ijumaa la kumtaka mbunge huyo kuelezea kinagaubaga kipi kimetokea hadi kufikia hatua ya kupoteza sifa za kuwa mbunge.

 

Advertisement